MAREKANI NA RUSSIA ZATOFAUTIANA

putin_and_obama_cd07e.jpg
Kutoka mabara sita viongozi wa nchi 20 zenye nguvu duniani walikutana Alhamis katika kasri ya Russia iliyojengwa karne ya 18 kujadilia namna ya kupiga jeki uchumi wa dunia.Lakini swala la Syria liligubika ajenda hiyo.
Rais Barack Obama aliwasili Russia Alhamis kwa mkutano huo wa kila mwaka lakini hatakuwa na mazungumzo ya moja kwa moja na mwenyeji wake rais wa Russia Vladmir Putin. Na swala linalotela tofauti baina ya viongozi hao wawili ni Syria.
Ama kwa hakika kinacholetea utata kwenye ajenda ya kiuchumi ni tishio la Washington la kufanya mashambulizi ya angani dhidi ya jeshi la Syria kwa matumizi yake ya silaha za sumu dhidi ya raia wake.Naibu waziri wa fedha wa China Zhu Guangyao alieleza wasiwasi wake juu ya kupanda kwa bei ya mafuta duniani ikiwa kutakuwa na hatua ya kijeshi dhidi ya Syria. Alisema endapo bei ya mafuta itapanda, uchumi wa dunia utadhurika.
Russia ni mshirika wa karibu wa China na Syria vilevile.Katika mkutano huo maafisa wa Russia walikariri msimamo wao wa kuelezea mashaka juu ya shtuma za Marekani dhidi ya Syria kwamba ilitumia gesi yenye sumu kuuwa zaidi ya raia wake 1400.
Msemaji wa rais Putin Dmitri Peskov aliongoza lawama hizo, akisema madai kuwa serikali ya Syria ilitumia gesi ya sumu dhidi ya wananchi wake "hayaaminiki."
Lakini maafisa wawili wa ngazi ya juu kutoka Jumuiya ya Ulaya walitoa shtuma kali dhidi ya serikali ya Syria kwa shambulizi la gesi ya sumu wiki mbili zilizopita. Rais wa tume ya Ulaya Jose Barroso alisema: "Hali hii ni doa katika nafsi ya walimwengu." Naye rais wa baraza la Jumuiya hiyo ya Ulaya Herman Van Rompuy alisema;" taarifa kutoka kwa vyanzo mbalimbali zinaashiria kuwa serikali ya Syria inawajibika kwa mashambulizi haya."
Wote wawili walisema suluhu pekee kwa mzozo wa Syria litakuwa la kisiasa.Naye waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Laurent Fabius aliiambia televisheni ya Ufaransa kuwa msimamo wa Ufaransa ni wa kuadhibu-- na kujadiliana. Alisema bila ya adhabu rais wa Syria Bashar al-Assad hataweza kujadilia mwisho wa vita hivi vya wenyewe kwa wenyewe ambavyo vimesababisha vifo vya zaidi ya watu laki moja.
Na wakati rais Obama alitoka nje ya gari lake la kifahari alikuwa na tabasamu kubwa kwa rais Putin lakini pembeni mwa kamera za wanahabari, wapambe wao walieleza kuwa hakuna mpango wa viongozi hao kuzungumza moja kwa moja.Na kabla ya kuondoka Stockholm kuelekea Russia Alhamis bw. Putin aliwaambia waandishi habari kuwa Marekani "imegonga mwamba" kwenye mahusiano yake na Russia.
Previous Post Next Post