MWENYEKITI wa Yanga SC, Alhaj Yussuf Mehboob Manji amesema hakuna mgawanyiko ndani ya klabu hiyo na habari kwamba Seif Ahmed 'Magari' ametengwa ni uzushi, lakini habari za ndani kutoka kwenye klabu hiyo zinasema uongozi unaamini unahujumiwa na
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF). (HM)
Kumekuwa na habari kwamba Seif Magari ameondolewa katika sehemu ya uongozi wa klabu na kwa sababu hiyo, hata swahiba wake, Abdallah Ahmed Bin Kleb ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano Yanga, naye amejitoa pia.
"Hakuna mgawanyiko, hayo ni maneno tu, Seif yupo na Majjid (Suleiman) wote tupo nao. Na hatuna wasiwasi na ligi, Simba SC inaongoza inatuzidi pointi tano tu.
Tumefungwa na Azam FC kwa bahati mbaya, sisi ndio tulicheza mpira mzuri na kila mtu ameona,"alisema Manji alipozungumza na BIN ZUBEIRY jana usiku.
Yanga imeambulia pointi sita katika mechi tano za mwanzo za Ligi Kuu, ikishinda moja, 5-1 dhidi ya Ashanti United, sare tatu za 1-1 na Coastal Union, Mbeya City na Prisons kabla ya kufungwa 3-2 na Azam FC juzi, wakati wapinzani wao wa jadi, Simba SC wapo kileleni kwa pointi zao 11, wakifuatiwa na Azam FC wenye pointi tisa.
Pamoja na hayo, habari za ndani ambazo BIN ZUBEIRY imezipata kutoka Yanga SC zinasema kwamba, klabu hiyo inaamini inahujumuwa na TFF kwa sababu ambazo wanaamini ni uongozi wa shirikisho hilo kuchukizwa na upinzani wa Yanga katika mambo kadhaa.
Mjumbe mmoja wa Kamati ya Utendaji ya Yanga amesema kwamba TFF inawahujumu kupitia marefa na katika mechi ambazo klabu hiyo imecheza ilionewa na waamuzi wazi wazi.
Mjumbe huyo amesema pia TFF wamewakomoa kwa kumfungia mchezaji wao Mrisho Ngassa ili kupunguza kasi yao katika mechi za mwanzoni za msimu.
"Sisi tunajua hila na njama zote za TFF, lakini hatuwezi kuwaambia lolote, zaidi tunajipanga kuendelea kucheza ligi katika mazingira magumu na mwisho wa siku tutatetea ubingwa wetu. Hatuna wasiwasi nao, viongozi wengi pale TFF siku zao zinahesabika, watatoka wataingia wengine na haki itarudi,"alisema.
Aidha, Mjumbe huyo amepinga kwamba Yanga inapinga Mkataba wa haki za matangazo ya Televisheni wa Azam TV, bali wanapinga TFF kuingia dili hilo kinyemelea bila kuzishirikisha klabu.
"Sisi tumecheza mechi na Mbeya City kule Mbeya mapato Milioni 100, sasa kama ile mechi inarushwa ina maana watu wengine wataangalia kwenye TV na mapato yatapungua, lazima sisi klabu tujue na turidhike kuhusu Mkataba, siyo wao TFF wafanye kwa niaba yetu, kwa sababu wao hawachezi ligi, ni sisi,"alisema Mjumbe huyo na kuongeza.
"Mimi ninakuambia, utaona, Azam TV watakapoanza kurusha mechi za Ligi Kuu mapato yatapungua. Mtu hawezi kutoka mbali kwenda Uwanja wa Taifa, wakati anaweza kuona mechi kwenye TV tena kwa ubora wa hali ya juu.
Sasa lazima klabu zipewe fedha ambazo hata watu wakipungua uwanjani hazitahisi maumivu. Lakini kwa hili sisi tunaonekana maadui na TFF wanatuhujumu, acha waendelee, lakini wataondoka muda si mrefu na haki itarudi,"alisema Mjumbe huyo.
Uchaguzi Mkuu wa TFF unatarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwezi ujao na Rais wa sasa wa shirikisho hilo, Leodegar Chillah Tenga hagombei, wakati Makamu wake wa kwanza, Athumani Nyamlani atagombea nafasi hiyo dhidi ya Jamal Malinzi, Katibu wa zamani wa Yanga SC.
Kuhusu Ngassa, mchezaji huyo amefungiwa mechi sita za mashindano adhabu ambayo alimaliza juzi kwa kosa la kusaini mikataba na timu mbili, Simba SC alikokuwa anacheza kwa mkopo kutoka Azam na Yanga SC alikohamia rasmi baada ya kumaliza Mkataba na Azam FC. Ngassa pia ametakiwa kurejesha Sh.
Milioni 30 alizochukua Simba SC kusaini Mkataba na kulipa fidia ya Sh. Milioni 15, jumla Milioni 45.
Katika hilo, Yanga SC wanalalamika kwamba Ngassa aliadhibiwa na Kamati ya Nidhamu ya TFF, bila ya kuitwa mwenyewe kuhojiwa kuhusu Mikataba hiyo- hivyo wanaamini hakutendewa haki.
Ngassa mwenyewe anasema kwamba Simba SC 'walimpiga change la macho'- akidai walimuambia apokee fedha hizo ili kukubalia kucheza kwao kwa mkopo, baada ya awali kugoma- lakini aliposaini akageuziwa kibao na kuambiwa amesaini Mkataba wa kuendelea kucheza kwa mwaka mmoja zaidi.
Ngassa anasema hata siku moja asingeweza kukubali kusaini popote kwa Sh. Milioni 30, kwa thamani yake ni zaidi ya Sh. Milioni 50 kwa msimu mmoja. Hata hivyo, Yanga SC imelainika na kukubali kumlipia mchezaji huyo Sh. Milioni 45 ili wiki hii aanze kucheza Ligi Kuu.
Credit: binzubeiry
Tags:
Sports