Adaiwa kuuawa Westgate
*Alifika Tanzania kwa Pasipoti ya Afrika Kusini
Ssamantha Lewthwaite, mwanamke wa Uingereza anayetajwa kuwa kiongozi wa ugaidi uliofanyika Nairobi, Kenya
WAKATI umwagaji wa damu katika kituo cha biashara cha Westgate ukiingia siku ya nne jana, Mwanamke ambaye ni raia wa Uingereza, Samantha Lewthwaite (29), anayetajwa kuwa ndiye aliyeongoza kundi la Al-Shabab kufanya shambulizi hilo, anahofiwa kuuawa. (HM)
Gazeti la Daily Mail la Uingereza, lilikariri vyanzo vyake vilivyoko ndani ya Jeshi na mfumo wa usalama nchini Kenya, ambavyo vimethibitisha kuwa mwanamke huyo ni miongoni mwa magaidi waliouawa na Serikali ya Kenya.
Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Amina Mohamed, katika mahojiano yake na kituo cha habari cha PBS, hakusema kama mwanamke huyo ameuawa lakini alithibitisha kuwa miongoni mwa magaidi waliovamia Westgate ni mwanamke wa Uingereza ambaye hata hivyo hakumtaja jina.
Hatua hiyo iliibua tetesi kwenye vyombo vya habari vya Kenya ambavyo vilimtaja mwanamke huyo kuwa ni Samantha.
Hata hivyo kauli hiyo ya Waziri huyo inaonekana kupingana na ile iliyotolewa awali na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Kenya, ambaye alisema kuwa magaidi wote waliovamia kituo hicho walikuwa wanaume na kwamba huenda baadhi yao walivalia mavazi ya kike.
SAMANTHA LEWTHWAITE
Mwanamke huyo anajulikana kwa jina la 'Mjane Mweupe,' inaelezwa yeye pamoja na baba yake, waliwahi kuwa wanajeshi nchini Uingereza.
Samantha ni mjane wa Jermaine Lindsay, ambaye alijilipua kwa bomu la kujitoa mhanga Julai 7, mwaka 2005 nchini Uingereza na kuua watu 52.
Baada ya tukio hilo, mwanamke huyo alidaiwa kulaumu hatua ya mumewe, lakini sasa yeye amefanikisha mpango wa kutekwa na kushambulia Westgate na alikuwa akitafutwa na majasusi wa Kenya kwa tuhuma za ugaidi.
Taarifa zilizochapishwa na Gazeti la nchini Uingereza la Daily Mail na pia zilizothibitishwa na Kundi la Al Shabab, liliwataja watekaji waliohusika katika tukio hilo la Kenya kuwa ni pamoja na Samantha Lewthwaite (29), ambaye alikuwa na magaidi wengine Ahmed Nasir Shirdoon (24) mkazi wa London (Uingereza), Jenerali Mustafe Noorduiin (27) mkazi wa Kansas City (Marekani) na Abdifatah Osman Keenadiid (24), mkazi wa Minneapolis (Marekani).
Wengine ni Ahmed Mohamad Isse (22) mkazi wa Saint Paul (Marekani), Ismael Guled (23) raia wa Finland, Abdirizak Mouled (24), mkazi wa Ontario, Canada, Zaki Jama Caraale (20), Sayid Nuh (25) raia wa Somalia na Liban Adam (23) raia wa Uingereza.
Samantha Lewthwaite ni nani?
Samantha Lewthwaite alizaliwa mwaka 1983, alibadili dini na kuwa Mwislamu mwaka 2002 na kuitwa Sherafiya, baada ya kuolewa na Lindsay.
Ametajwa kuwafundisha wanawake wote wanaojihusisha na ugaidi katika kambi mbalimbali za magaidi. Maisha yake yalianza katika mitaa ya Aylesbury, mjini Buckinghamshire, London nchini Uingereza.
Miaka nane tangu kufiwa na mumewe, Samantha amegundulika kuwa miongoni mwa watu wanaojihusisha na kundi la Al Qaeda kwa upande wa Afrika Mashariki, huku akiwa na cheo cha msemaji mkuu.
Ugaidi wa Samantha Lewthwaite
Mwanamke huyo anatajwa kuhusika na tukio la kigaidi katika ubalozi wa Uingereza nchini Yemen na amekuwa kiunganishi cha kundi la Al Qaeda Afrika Mashariki.
Mwaka 2005, alihusika na mlipuko wa bomu lililoua watalii mjini Mombasa, nchini Kenya.
Desemba mwaka 2011, akiwa na gaidi Jermaine Grant, walikamatwa baada ya kugundulika kupanga mikakati ya kigaidi, lakini alifanikiwa kutoroka, huku Grant akisubiri kesi yake nchini Kenya.
Tangu wakati huo amekuwa akisakwa huku na huko na maofisa usalama bila mafanikio, huku akiendelea kuchangisha fedha za kufanyia ugaidi.
Ofisa mwandamizi wa Usalama Kenya alisema: "Tunaamini Samantha alikuwa akiongoza operesheni hii, lakini mustakabali wake hatuwezi kuwaambia sasa. Lakini tunathibitisha alikuwa kati ya magaidi."
Familia ya Lewthwaite
Wanafamilia ya Lewthwaite wamesema kuwa kwa muda mrefu hawana mawasiliano yoyote na gaidi Samantha Lewthwaite.
Wamesema kuwa Samantha aliacha kuwasiliana na familia yake tangu akiwa na mjamzito wa miezi 7, wakati mumewe Jermaine Lindsay alipofanya shambulio la kigaidi mwaka 2005. Mwanamke huyo alijulikana zaidi kwa jina la 'Dada Mzungu' kwa wafuasi wake.
Makachero wa MI6 waisifu Kenya
Katika hatua nyingine, Shirika la Kijasusi la Uingereza, Military Inteligency (MI6), limesema Jeshi la Kenya linastahili sifa kutokana na ufanisi walioonyesha wakati wakipambana na magaidi.
Majasusi wa MI6 walisema wanajeshi wa Kenya walifanikiwa kuingia ndani ya jengo la Westgate bila msaada kutoka majeshi ya nje.
Kwa mujibu wa Gazeti la Daily Mail, Samantha Lewthwaite anadaiwa kuvaa vazi la kujifunika mwili mzima, huku akitembelea nchi za Somalia, Kenya na Tanzania.
Miongoni mwa waliouawa katika shambulio hilo ni Daktari mashuhuri duniani, Dk. Juan Jesus Ortiz-Iruri (63), ambaye ni raia wa Peru.
Afrika Kusini yamchunguza
Katika hatua nyingine, Serikali ya Afrika Kusini imetangaza kufanya uchunguzi kuhusu kuwapo kwa taarifa kuwa Samantha Lewthwaite alikuwa akitumia hati ya kusafiria ya nchi hiyo.
Lewthwaite anadaiwa kutumia jina la bandia la Natalie Faye Webb, ambalo limekutwa katika maiti yake ndani ya jengo la Westgate.
Credit: mtanzania
Tags:
Social