Tukio la Westgate halitasahaulika kirahisi kutokana na jinsi ambavyo limechukua uhai wa watu wasio na hatia kikatili na kusababisha maumivu kwa wale walionusurika na shambulio hilo. Unapopata nafasi ya kusikia watu walionusurika kuuawa katika shambulio hilo ndio unaweza kujua ukubwa wa tukio hilo.
Ikiwa inaelekea wiki moja tangu shambulio hilo litokee katika jengo la biashara Westgate jijini Nairobi, watu mbalimbali wamehadithia jinsi walivyoshuhudia kilichotokea wakati wa tukio hilo mpaka walipofanikiwa kujiokoa au kuokolewa.
Mashuhuda wanasema kuwa magaidi hawakuishia tu kushambulia raia na wana usalama kwa silaha, lakini waliwatesa pia kwa kuwang’oa macho, vidole kwa koleo (pliers) na kuwanyonga kwa kuwaning’iniza miili yao kabla ya kuwauwa.
Mfano wa Koleo (Pliers) iliyotumiwa na magaidi kuwang’oa mateka vidole, macho, na pua
Jana, wanajeshi na madaktari ambao walikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kuingia Westgate toka shambulio hilo kumalizika Jumanne, walielezea jinsi mateka walivyopata mateso kutoka kwa magaidi kuwauwa.
Kwa mujibu wa Mail Online wanajeshi waliokuwa wakipambana na magaidi hao wamesema kuwa miili ya watoto ilikutwa katika majokofu ya chakula baada ya kuuwawa kikatili huku visu vikiwa bado katika miili yao.
“Unakuta watu wamenyongwa kwa kuning’inizwa kutoka kwenye paa” alisema daktari ambaye hakutaka jina lake litajwe.
“Waliwatoa macho, masikio na pua, kisha wakawachonga vidole kama penseli kisha kuwaambia waandike majina yao kwa damu inayotoka kwenye vidole”.
“Kwa kweli kama ukiiangalia miili yote, ukitoa ya wale ya waliofanikiwa kuokolewa, wengi vidole viling’olewa na pliers, na pua ziling’olewa na pliers.” alisema.
Mfanyakazi wa Radio Africa Group ya Kenya Bernard Wambua ni mmoja kati ya waathirika wenye bahati baada ya kupona katika shambulio hilo bila hata mchubuko mmoja.
Wambua akiongea na Daily Nation alisema yeye alifanikiwa kumuona uso kwa uso mwanamke wa Uingereza Samantha Lewthwaite aka ‘The White Widow’ anayehisiwa kuongoza shambulio hilo, na kudai aliwashambulia na kuwaongoza magaidi wenzake aliokuwa nao kwa kuwaonyeshea watu wa kuwapiga risasi.
Samantha ‘White Widow’
“Nilimwona mwanamke mweupe akiwa amevaa kibegi cha pesa kiunoni. Alimimina risasi kuja tulipokuwa bila kujali kelele za mayowe ya watoto”. Alisema
Wambua aliendelea kusema kuwa yeye pamoja na wenzake wengine 50 kutoka East FM walikuwa eneo la maegesho ya magari katika jengo la Westgate wakiandaa shindano la kupika la watoto, ambapo watoto waliohudhuria walisindikizwa na wazazi wao.
Kwa mujibu wa Wambua mambo yaliendelea vizuri mpaka saa 5 na dakika 50 asubuhi ya Jumamosi (September 21),
“Tulikuwa ndio tunamalizia kuandaa meza ambayo ndiyo ingetumiwa na watoto kwaajili ya shindano la kupika muda mfupi kabla ya saa sita mchana tulipoanza kusikia milio ya risasi. Mwanzo tulidhani ni wizi tu wa kawaida lakini sauti za milio ya risasi ziliendelea kuwa kubwa kama mtu anayepiga anakuja tulipokuwepo.
Wanaume wawili walikuja kwenye eneo la maegesho ya magari tulipokuwepo, walikuwa wamevaa t-shirt na jeans na mmoja aakiwa amejifunga kiremba cha kiarabu kichwani. Mikononi walikuwa na silaha nzito na niliona bastola zikitokeza pia mifukoni mwao, walianza kushambulia kwa kumpiga risasi kila mtu na kila kitu.
Wengi wetu tulijificha chini ya meza tulizokuwa tunaandaa kwaajili ya shindano, lakini magaidi waliendelea kutushambulia.
Hati feki ya kusafiria ya Samantha ‘White Widow’
Na hapo ndipo mwanamke ngozi nyeupe alipoungana nao, yeye pia alikuwa na bunduki. Alikuwa anawaonyesha vitu na wenzake kuvipiga risasi. Mwanamke huyo aliupiga risasi mtungi wa gesi tuliokuwa tunautumia ambao ulisababisha moto mdogo kutokea. Bahati nzuri haukusambaa, lakini aliendelea kushambulia microwaves zilizokuwepo. Yeyote aliyepiga yowe alipigwa risasi na magaidi hao.
Waliondoka eneo la maegesho ya magari baada ya kuwa kimya kabisa, labda wao walidhani kuwa wamewauwa watu wote. Kulikuwa na ukimya wa kutisha, na harufu nzito ya damu, watu wengi waliuwawa.” Alisema Wambua
Baada ya vyombo vya usalama vya Kenya kufanikiwa kukabiliana na magaidi hao, Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta alitangaza siku tatu za maombolezo kuanzia jumatano ya wiki hii.
Magaidi kati ya 10 na 15 wanahisiwa walivamia Westgate Jumamosi iliyopita, kulingana na taarifa ya viongozi wa Kenya.
SOURCE: GHAFLA, MAIL ONLINE