YANGA WAWASILISHA RUFAA TFF LEO KUPINGA ADHABU ZOTE ZA NGASSA



5_2d9a3.jpg

Bin Kleb kushoto akikumbatiana na Ngassa baada ya kusaini Yanga SC. Kulia ni Mjumbe wa Kamati ya Mashindano ya Yana SC, Mussa Katabaro
YANGA SC jana imewasilisha Rufaa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kupinga adhabu ya mshambuliaji wake, Mrisho Khalfan Ngassa kufungiwa mechi sita na kutakiwa kuilipa klabu yake ya zamani, Simba SC Sh. Milioni 45.

Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga SC, Abdallah Ahmed Bin Kleb ameiambia BIN ZUBEIRY jioni hii kwamba, mawakili wao watatu leo wamewasilisha Rufaa hiyo TFF ikiwa imebeba hoja nzito, ambazo wanaamini zitatosha kumkomboa Ngassa.
"Mawakili wetu nadhani watakuwa na Mkutano na Waandishi wa Habari kuzungumzia Rufaa waliyowasilisha, kwa kweli katika hili suala mchezaji hajatendewa haki, nasi tunawajibika kumsaidia,"alisema Bin Kleb.
Tutapambana hadi kieleweke;
Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF, ilimuidhinisha Ngassa kuchezea Yanga baada ya kukamilisha usajili wake, kufuatia kupitia usajili wa wachezaji wa klabu za Ligi Kuu ya Vodacom msimu huu wiki iliyopita.
Hata hivyo, Kamati hiyo chini ya Mwenyekiti wake Alex Mgongolwa ilibaini kuwa Ngassa alisaini mkataba mwingine Simba (katika kipindi ambacho alikuwa na mkataba na Azam) ambapo anatakiwa kurejesha fedha alizopokea (sh. milioni 30) pamoja na fidia ya asilimia 50 (sh. milioni 15) ya fedha hizo kwa Simba.
Kamati hiyo pia ilimfungia mechi sita za mashindano na kumtaka awe amelipa fedha hizo ndani ya kipindi hicho cha kukosa mechi hizo na akishindwa, hataruhusiwa kucheza hadi atakapolipa fedha hizo.
Ngassa alisaini Yanga baada ya kuitumikia Simba SC kwa mwaka mmoja akitokea Azam FC, akiwaambia viongozi wa Jangwani amemaliza Mkataba wake Msimbazi.
Lakini baadaye Simba SC ikaibua Mkataba iliyosaini na Ngassa na inaonyesha anatakiwa kufanya kazi Msimbazi kwa mwaka mmoja mwingine.
TFF nayo ikathibitisha, inao Mkataba ambao Ngassa alisani na Simba SC.
Hoja kuu ya Yanga katika Rufaa yao ni kitendo cha Simba SC kumsainisha Ngassa Mkataba wakati imemchukua kwa mkopo kutoka na Azam na bado alikuwa ana Mkataba na klabu hiyo- na kwa kuwa wanaamini hilo ni kosa kwa mujibu wa kanuni, wanapingana na adhabu alizopewa.
Previous Post Next Post