Ofisa Usalama Uwanja Wa Ndege Mkoani Kigoma Anaswa Akivusha Madini ya Dhahabu Bila Kuwa na Kibali, Soma zaidi..


kigomaAIRPORT_82b58.jpg
Jeshi la Polisi na Idara ya Madini, mkoani Kigoma, limemnasua kiaina ofisa usalama wa uwanja wa ndege, Cleophace Lukindo, aliyedakwa na maofisa wenzake akivusha madini ya dhahabu bila kuwa na vibali.
Tukio hilo lilitokea Agosti 22 uwanjani hapo wakati Lukindo akitaka kupita bila kukaguliwa tayari kwa ajili ya kusafirisha madini hayo kwa ndege ya Shirika la Ndege Tanzania kuelekea jijini Dar es Salaam ndipo wenzake wakamtilia mashaka na kumkamata.
Madini hayo yalikuwa na uzito wa kilogramu tisa huku thamani yake ikielezwa kuwa takriban sh milioni 400.
Kwa mujibu wa vyanzo vyetu, tukio hilo limekuwa likifichwa na uongozi wa uwanja pamoja na jeshi la polisi mkoani humo kwa kile kinachodaiwa kuwa ofisa huyo amekuwa akitoa vitisho kwa wafanyakazi wenzake.
Katika hatua ya kushangaza gazeti hili jana lilidokezwa kuwa madini hayo yamekabidhiwa na idara ya madini kwa raia mmoja wa Jamhuri ya Kidemkrasia ya Congo (DRC) baada ya kutozwa faini kutokana na kitendo hicho cha kutaka kuyavusha kinyemela.
Hata hivyo, taarifa hizo zimekuwa za kukinzana kati ya meneja uwanja, Tesha, na Kamanda wa Polisi, Frasser Kashai.
Wakati Tesha akidai waliyakabidhi madini hayo polisi pamoja na mtuhumiwa, Kashai alisema kuwa Idara ya Madini Kigoma ndiyo iliamua kuyarudisha madini hayo kwa mmiliki huyo raia wa DRC.
"Unajua sisi hatushughuliki na madini, tulipomkamata mtuhumiwa tulimhoji kwa kushirikiana na watu wa madini lakini kwa taratibu zao walimtoza faini raia huyo kwa kutaka kuyavusha bila kuwa na leseni kwa kumtumia ofisa huyo," alisema.
Kashai aliongeza kuwa Idara ya Madini ilithibitisha kuwa raia huyo wa DRC anayo lesini ya umiliki wa madini hayo lakini kosa lake hakuwa na vielelezo vya kuyasafirisha.
Alisema kwa sasa wao wanaendelea na utaratibu wa kumchunguza ofisa huyo kwani wakati wa kukamatwa kwake alifanya fujo ya kumjeruhi mwenzake na kuvunja kufuli.
Kwa mujibu wa chanzo chetu cha habari, ofisa huyo anadaiwa kuwekewa mtego na maofisa wenzake wawili baada ya kubaini mpango wake huo wa kutaka kuvusha mzigo huo kwa kutumia lesini ya mtu mwingine.
Taarifa zilidokeza kuwa ofisa huyo licha ya kuwa na leseni hiyo isiyokuwa ya kwake, hakuwa na nyaraka zingine za kuonyesha alikopata mzigo, anaupeleka wapi na kiasi chake.
Chanzo hicho kilidokeza kuwa baada ya kufika eneo la ukaguzi, ofisa mwenzake, Yusuf Mpame, na askari polisi Koplo Theophil walimtaka aonyeshe vibali na nyaraka hizo ili wathibitishe kuwa mzigo huo ulikuwa unasafirishwa kihalali.
Hata hivyo, Lukindo baada ya kuona wenzake wamemshtukia na kutaka kumkamata alitumia nguvu kumkaba ofisa mwenzake Mpame ambaye alimnyonga shingo na kisha kung'ata lakini akanusuriwa na Koplo Theophil na Jeremiah.
Previous Post Next Post