Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alisema Serikali inaangalia uwezekano wa kuondoa zuio la mabasi ya abiria kutembea usiku kama ilivyo kuwa miaka ya nyuma. Kauli hiyo aliitoa bungeni jana alipokuwa akijibu maswali katika kipindi cha maswali ya papo kwa papo ambacho kimekuwa kikifanyika kila Alhamisi pindi waziri mkuu anapokuwapo bungeni.(P.T)
Waziri Pinda alisema bado inahitajika elimu zaidi kwa madereva wa mabasi hayo, kwani ni lazima kuwepo kwa madereva wawili katika kila basi ili waendeshe kwa kubadilishana.
"Ni kweli kulikuwa na zuio hilo lakini lilitokana na kuongezeka kwa ajali na hasa wakati wa usiku, lakini kwa sasa kuna uboreshaji wa miundombinu tunaweza kuangalia jinsi gani ibadilishwe," alisema.
Wakati huo huo, Pinda alisema Serikali itachukua kila tahadhari kuhakikisha vitambulisho vya taifa vinatolewa kwa kila Mtanzania kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Pinda alitoa ahadi hiyo wakati akijibu swali la Mbunge wa Mkanyageni, Mohamed Habib Mnyaaa (CUF), aliyetaka kujua hatua ya Serikali katika kuhakikisha vitambulisho hivyo vinatolewa kwa wakati.
Pinda alisema nia ya Serikali ni kuhakikisha kuwa vitambulisho hivyo vinapatikana kwa wakati ili viweze kutumika katika uchaguzi kama ilivyoahidiwa awali.
"Moja ya tahadhari hizo ni pamoja na kuongeza wigo wa utoaji wa vitambulisho hivyo ili wananchi wengi zaidi waweze kupata vitambulisho hivyo.
"Tunatumia njia mbalimbali ambazo tayari tumeziweka kama tahadhari endapo suala la utoaji wa vitambulisho halitakamilika, lakini ni matumaini yetu suala hili litakamilika kama lilivyopangwa," alisema.
Tags:
Social