Brand Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager Bw. George Kavishe (wa tatu kulia) akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi rasmi wa ziara ya matamasha ya muziki ijulikanayo kama ‘Kili Music Tour 2013’ iliyoanza tangu tarehe 22 Juni 2013.
Tanzania Breweries Limited (TBL) chini ya nembo yake ya Kilimanjaro Premium Lager, inangoa nanga kwa awamu ya pili ya ‘Kili Music Tour 2013’ wikiendi hii mjini Mwanza.
Tamasha hili kubwa litafanyika Jumamosi ya tarehe 17 Agosti, 2013 mjini Mwanza kwenye uwanja wa CCM Kirumba na litajumuisha wasaniii 11 ambao ni Diamond, Snura Mushi, Professor J, Lady Jay Dee, Roma, Dabo, Bob Junior,Ben Pol, Kala Jeremiah, Fid Q na AT.
Matamasha ya Kili Music Tour 2013 yalikuwa yamepumzika kwa muda wa mwezi mmoja na yanarejea tena kwa kishindo kwenye mikoa mitano iliyobaki.
“Tunashukuru kuwa watanzania wamepokea tamasha hili kwa moyo mkunjufu kabisa na walishiriki kikamilifu kwenye mikoa ya Dodoma, Tanga na Kilimanjaro, tuliamua kupumzika kwa muda wa mwezi mmoja kwa ajili ya mfungo, na hii ilitupa muda mzuri wa kujipanga na kuboresha zaidi matamasha haya hivyo basi tunategemea Mwanza itajumuika nasi ipasavyo kufanikisha tamasha litakalofanyika mkoani hapo siku ya Jumamosi ya tarehe 17 mwezi huu wa nane.” Alisema bwana George Kavishe meneja wa bia ya Kilimanjaro.
Bwana Kavishe aliendelea kufafanua kuwa “bia ya Kilimanjaro Premium Lager inaendelea kutoa bonge la kiburudisho kwa watanzania kwa kuhakikisha kuwa kila mkoa unapelekewa wasanii mahiri kabisa wa muziki wa bongo fleva hivyo mashabiki wa muziki wakae mkao wa burudani.
Kwa niaba ya wasanii wenzake msanii mahiri wa bongo fleva Professor Jay “Joseph Haule” amewataka wakazi wa Mwanza kujitokeza kwa wingi akisema “tumejiandaa vizuri sana kutoa burudani kali kabisa, lazima mji wa Mwanza utikisike kwa kishindo cha bonge la kiburudisho kwa style tuipendayo ya “kikwetukwetu”.
Tags:
Entertainment