Laptop za Ubuntu zinazotumia nishati ya jua ‘Solar’ zinatarajiwa kuzinduliwa barani Afrika mwishoni mwa mwaka huu.
Watengenezaji wa Ubuntu solar powered Laptop kutoka nchini Canada kampuni ya WeWi, wamesema zinauwezo wa kukaa na umeme kwa muda wa masaa 10 kabla ya kuhitaji kuchajiwa tena na zinachukua masaa mawili tu kuchaji betri hadi ijae zinapopata mionzi ya jua.
Bara la Afrika ndio litakuwa lakwanza kufaidika na laptop hizo za Solar, na kufuatiwa na Mashariki ya kati, kisha Ulaya na baadaye Marekani Kusini na Kaskazini ndio wataweza kuzipata laptop hizo.
Laptop hizo zimetengenezwa kwaajili ya maeneo kama ya kijeshi pamoja na nchi zinazoendelea hususan maeneo ambayo bado hayajapata huduma za umeme.
Kwa mujibu wa mtandao wa News Discovery hii ndio laptop ya kwanza inayotumia nishati ya jua, japokuwa mwaka 2011 Samsung waliwahi kuja na laptop inayotumia jua Samsung NC215S netbook lakini haikuwa na uwezo wa kukaa masaa 10 na ilikuwa na panels ndogo.
Ubuntu solar powered Laptops zitazinduliwa nchini Ghana mwishoni mwa mwaka huu na zitapatikana kwa kuanzia $350 (566,000 Tsh)