Inaonekana vita dhidi ya biashara haramu ya madawa ya kulevya ni ngumu. Katika mwezi July pekee Watanzania watano wameshakamatwa wakisafirisha madawa hayo.
Tukio la kwanza ni la wasichana wawili ambao tayari wamefahamika majina yao (kwa mujibu wa gazeti la NIPASHE) kuwa ni Agnes na Melisa waliokamatwa kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa O.R. Tambo jijini Johannesburg, Afrika Kusini waliokuwa na kilo 150 za madawa hayo ( crystal methamphetamine).
Madawa hayo yanayojulikana kama “tik” yana thamani ya dola milioni 4.3 za Kimarekani sawa na shilingi bilioni 7 za Tanzania, kwa mujibu South Africa Revenue Service (SARS).Kiwango hicho ni kikubwa zaidi kuwahi kukamatwa kwenye uwanja wowote ule wa ndege nchini humo.
Katika tukio jingine Jumamosi iliyopita, watu wawili walikamatwa kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam wakiwa na kilo mbili za madawa aina ya heroin yenye thamani ya shilingi miloni 90.Kwa mujibu wa mkuu wa kitengo cha polisi cha kuzuia biashara ya madawa ya kulevya nchini Godfrey Nzowa.
Wawili hao walikuwa wakielekea Bangkok.
Tukio jingine ni la mwanamke mwenye miaka 34 aliyekamatwa wiki iliyopita kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa wa Harare nchini Zimbabwe akiwa na madawa ya kulevya yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 72 akitokea nchini India. Mollel Jackline Richard, anayeishi nchini Afrika Kusini anashikiliwa nchini Zimbabwe ambapo kesi yake itasomwa July 27.
Mtanzania huyo alikamatwa na kilo 15 za madawa aina ya ephedrine.