Mshambuliaji, Edinson Cavani (HM)
HATIMAYE Paris St Germain imekamilisha usajili wa mchezaji ghali, mshambuliaji wa Napoli, Edinson Cavani kwa ada ya uhamisho ya Pauni Milioni 55 kwa Mkataba wa miaka mitano.
Cavani amekuwa akiwaniwa na klabu kadhaa kubwa Ulaya majira haya ya joto, zikiwemo Manchester City, Chelsea na Real Madrid nazo zilihusishwa na kugombea saini ya mshambuliaji huyo wa Uruguay.
Pamoja na hayo, mabingwa wa Ufaransa walipiga kasi wiki iliyopita na jana mchana wametangaza rasmi kwenye tovuti yao kwamba wamemsajili mchezaji huyo.
Cavani amekuwa tishio tangu ajiunge na Napoli akitokea timu nyingine ya Italia, Palermo Julai 2010, akifunga mabao 104 katika mechi 138 alizocheza Partenopei.
Aliisaidia mno Napoli kushika nafasi ya pili katika Ligi Kuu Italia, Serie A akiibuka mfungaji bora kwa mabao yake 29.
Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 26 anayesajiliwa kwa bei mbaya zaidi majira haya ya joto, anaungana na wachezaji wengine bora waliosajiliwa awali na timu hiyo, Zlatan Ibrahimovic, Marco Verratti, Ezequiel Lavezzi, Lucas Moura, Javier Pastore na Thiago Silva.
Cavani anatarajiwa kutengeneza pacha kali ya ushambuliaji kwa pamoja na Ibrahimovic, ambaye alishinda tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka wa Ligue 1 baada ya kufunga mabao 30 msimu uliopita.
Kocha mpya wa PSG, Laurent Blanc pia atatumai Cavani na mchezeshaji Lavezzi wataendeleza ushirkkiano wao mzuri waliokuwa nao Napoli.
Chanzo: binzubeiry