Mshauri wa Ufundi wa Tabora Marathon 2013, Tullo Chambo, (kushoto), akionesha baadhi ya zawadi zitakazotolewa kwa washindi wa mbio hizo zitakazofanyika Juni 22 mjini Tabora, katika hafla iliyofanyika mgahawa wa Yami Yami jijini Dar es Salaam jana.
KAMATI ya Mashindano ya Riadha ya Tabora Marathon, imezindua rasmi mbio hizo huku ikitangaza maboresho zaidi, ikiwamo fedha taslimu na zawadi ya vikombe na medali kwa washindi wa kwanza hadi wa tatu wa mashindano hayo yanayofanyika kwa mwaka wa pili sasa.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mshauri wa Ufundi wa Tabora Marathon, Tullo Chambo, alisema licha ya maboresho, mbio za mwaka huu zitakuwa kama za mwaka jana, ambazo ni km 21 wanaume, km 16 wanawake na km 5 kwa watu wazima na watoto.
Chambo ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Chama cha Riadha Tanzania (RT), alisema, mbio hizo mwaka huu, zitafanyika Juni 22, ambayo pia ni siku ya Olimpiki Duniani, ambako kitaifa itafanyika jijini Mbeya, hivyo itakuwa ni nafasi pia kwa wadau wa michezo Kanda ya Magharibi, kuiadhimisha siku hiyo kwa kushiriki mbio hizo.
"Licha ya aina ya mbio kuwa kama mwaka jana, maboresho yetu yako katika zawadi, ambapo washindi wa kwanza hadi wa tatu wataibuka sio tu na fedha taslimu kama mwaka jana, bali pia watapata vikombe na medali za Dhahabu, Fedha na Shaba," alisema Chambo.
Aliongeza kuwa, kwa kutambua historia ya mkoa wa Tabora katika Riadha, Kamati yake imeona umuhimu wa kuitumia fursa hiyo kuwekeza mchango wao katika mchezo huo, ili kuwanufaisha wakazi wa mkoa huo, lakini pia taifa kupata wanariadha watakaoliletea sifa.
Aidha, Mratibu wa Mashindano hayo, Ramadhani Makula, aliwashukuru wadau muhimu kwa kusaidia harakati za kuifikisha Kamati yake ilipo kimichezo, huku akiwataja baadhi yao kuwa ni Mkurugenzi wa NGS CO. Ltd ya Simiyu Njalu Silanga na Emmanuel Mwakasaka wa Tabora mjini
Wengine waliotajwa kutoa mchango uliotukuka kwa Kamati ya Tabora Marathon ni pamoja na Hamisi Kigwangala (Mbunge wa Nzega), Sarah Ramadhani wa Dar es Salaam, mwanariadha Banuelia Brighton na Taasisi ya Filbert Bayi Foundation.
Makula akazitaka taasisi, kampuni na wadau mbalimbali wenye nia ya dhati ya kuleta maendeleo ya michezo hasa riadha kujitokeza kudhamini Tabora Marathon, ili kuibua na kuindeleza vipaji vya mchezo huo, kwa mkoa ambao ulisifika kutoa wanariadha mahiri.