Meneja wa kampuni ya bia ya TBL George Kavishe akikabidhi mfano wa hundi ya sh. milioni 25 kwa katibu mkuu wa Yanga Lawrence Mwalusako
Mabingwa wa ligi kuu soka Tanzania bara na mabingwa watetezi wa kombe la Kagame, klabu ya Yanga ya Dar es salaam wamepewa zawadi ya sh. Milioni 25 kutoka kwa wadhamini wakuu wa klabu hiyo, Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), wameizawadia klabu hiyo Sh. Milioni 25 kwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Bara uliomalizika mei 18 mwaka huu.
TBL, wanaoidhamini Yanga na Simba kupitia bia ya Kilimanjaro Premium Lager imekabidhi mfano wa hundi ya Sh. Milion 25 leo kwa Yanga katika hafla iliyofanyika ukumbi wa Safari Pub, uliopo makao makuu ya TBL, Ilala, Dar es Salaam.
Meneja wa bia ya Kilimanjaro Premium Lager, George Kavishe wakati akikabidhi mfano wa hundi hiyo alisema Kilimanjaro Premium Lager imefurahishwa sana na ubingwa wa Yanga na kusema imejizatiti kikamilifu kuisaidia timu ambayo imeibuka bingwa katika ligi yenye ushindani mkubwa kutokana na kuibuka kwa timu mpya zenye nguvu.
“Yanga imekuwa akionesha soka safi kwa kipindi chote, ligi ni ngumu sana lakini wamecheza soka maridadi, hivyo kuibuka mabingwa sio ajabau kabisa. Napenda kuwapongeza wachezaji wa Yanga, kocha na Uongozi mzima wa Yanga kwa matokeo mazuri ya kushinda Ligi kuu kwa mara ya 24 sasa.” Alisema Kavishe.
Kavishe aliongeza kuwa zawadi hiyo ni sehemu ya sh bilioni 1.5 ya udhamini wa Kilimanjaro Premium Lager kwa Yanga na imetolewa kwa lengo la kuhamasisha klabu kujitahidi kwa ushindi zaidi na kusaidia klabu katika maandalizi yake kwa ajili ya mashindano ya kimataifa ambayo tayari Yanga ina sifa za kushiriki kutokana na ubingwa waliojipatia.
Akipokea hundi hiyo, Katibu mkuu wa Yanga , Bwana Lawrence Mwalusako alisema Yanga inaishukuru sana Kilimanjaro Premium Lager kwa mchango wao. Aliongeza kuwa Yanga ni timu nzuri na yenye nguvu kutokana na uongozi imara pamoja na udhamini mkubwa kwa bia ya Kilimanjaro Premium Lager.
‘‘Mafanikio yetu ya uwanjani ni kielelezo cha mafanikio ya kampuni na pia (TBL) na bia ya Kilimanjaro Premium Lager kwa ujumla ambayo imekuwa ikitusaidia sana.’’ alisema Mwalusako.
Mwalusako aliongeza kuwa kwa sasa Yanga ina nafasi ya kuonekana kwenye jukwaa la kimataifa la soka kutokana na mafanikio hayo na kuahidi kujipanga zaidi kufanbya makubwa zaidi.
Yanga itawakilisha Tanzania katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika na Kombe la Kagame.