TAARIFA YA CCM KWA VYOMBO VYA HABARI




Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi,Nape Moses Nnauye


Mei 19, 2013 Chama Cha Mapinduzi kilifanya kikao cha siku moja na wabunge wanaotokana na CCM, kikao hicho kilifanyika mjini Dodoma ambapo pamoja na viongozi wengine wa juu wa CCM kikao hicho kilihudhuriwa pia na Mwenyekiti wa CCM Rais Jakaya Mrisho Kikwete.


Kikao hicho kilikuwa na lengo la wabunge wa CCM na viongozi wa CCM wakiongozwa na Mwenyekiti wa Taifa wa CCM ambaye pia ni Rais na mtekelezaji mkuu wa Ilani ya uchaguzi ya CCM kubadilishana uzoefu wa namna ilani ilivyotekelezwa hasa kwenye majimbo kwa kipindi cha nusu ya muhula wa miaka mitano. Baada ya kubadilishana mawazo uliwekwa mwelekeo wa namna bora ya kutekeleza ilani na ahadi mbalimbali kwa kipindi kilichobaki.


Kwahiyo kwa kifupi lengo la kikao hicho ilikuwa ni kutathimini utekelezaji wa ilani majimboni na kuangalia namna bora ya kuweka msukumo mpya na mkubwa zaidi kwa kipindi kilichobaki cha utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM kwa 2010/2015, lengo likiwa kuhakikisha ilani na ahadi za CCM na wagombea wake zinatekelezwa kwa kiwango kikubwa.


Hata hivyo baada ya semina hiyo baadhi ya vyombo vya habari vimenukuu kauli inayodaiwa kutolewa na Mwenyekiti wa CCM Dr. Jakaya Kikwete kuwa ameruhusu wanaokusudia kuomba ridhaa ya CCM kugombea Urais wa 2015 kufanya kampeni.


CCM imesikitishwa na nukuu hiyo ya kupotosha ukweli wa kilichojadiliwa na hivyo tumelazimika kutoa ukweli wa kilichojiri na kujadiliwa. Ni kweli kuwa mjadala juu ya watu mbalimbali wanaotajwa au wanaojitaja kuwa na nia ya kugombea nafasi mbalimbali hasa udiwani, ubunge na Urais ulikuwepo na ulikuwa mkali.


Hata hivyo hitimisho la kikao na majumuisho ya Mwenyekiti wa CCM Taifa lilikuwa ni kukemea kwa nguvu zote pirika hizo na uvunjifu huu wa makusudi wa kanuni za Chama chetu ambazo kimsingi pirika hizi zinakigawa Chama na kuvuruga mshikamano na umoja ndani ya Chama.


Nasisitiza nukuu hiyo ya baadhi ya vyombo vya habari si sahihi na ni ya kupotosha ukweli. Inaelekea kuna kikundi cha watu wanamgombea wao wa kuchonga ambaye bila shaka anapungukiwa na sifa, hivyo wanajaribu kumuongezea sifa kwa kumlisha Mwenyekiti maneno na kuwaapa baadhi ya waandishi, uhuni huo haukubaliki.


CCM ina kanuni na taratibu zake zinazoisimamia na kuiongoza katika kufanya shughuli zake mbalimbali zikiwemo za mchakato wa kuwapata wagombea wake katika ngazi mbalimbali kuanzia shina hadi taifa.


Kanuni hizo ni pamoja na kanuni za Uteuzi wa wagombea wa CCM kuingia katika vyombo vya dola toleo la Februari, 2010 na Kanuni za uchaguzi wa CCM, toleo la 2012.


Katika Kanuni za Uchaguzi wa CCM Toleo la 2012 kanuni za jumla Ibara ya 33 inazungumzia Miiko ya kuzingatiwa wakati wa shughuli za uteuzi na uchaguzi. nanukuu“ Maadili na nidhamu ya chama katika kusimamia na kutekeleza shughuli za uchaguzi wa chama lazima kuzingatiwa na wale wote wanaohusika. Hivyo yawapasa kuelewa na kutambua kuwa;-


(1). “….wanachama wenye nia ya kugombea hawaruhusiwi kufanya kampeni ya aina yoyote kabla ya majina yao kuteuliwa na kikao kinachohusika”.


(4). “Ni mwiko kwa kiongozi au mwanachama yeyote wa CCM kuunda vikundi visivyo rasmi ndani ya chama, au kushiriki katika kampeni za uchaguzi za chini chini kinyume na ratiba ya uchaguzi na taratibu rasmi zilizowekwa”.


Ibara hiyo ya 33 kifungu kidogo cha 1 na 4 vinaweka wazi msimamo wa kikanuni wa Chama. Hivyo basi kwa mujibu wa kanuni za Uteuzi wa wagombea wa CCM kuingia katika vyombo vya dola toleo la Februari, 2010 na Kanuni za uchaguzi wa CCM, toleo la 2012 na kwa mujibu wa maagizo yaliyotolewa na kupokelewa kwenye kikao cha Mwenyekiti wa CCM Taifa na wabunge wa CCM mjini Dodoma tarehe 19/05/2013;


Ni marufuku kwa mwanachama yeyote wa CCM anayetaka kuomba CCM impe nafasi ya kugombea kwenye uchaguzi wa dola kujipitishapitisha na kuita wapiga kura na kukutana nao kinyume na kanuni za Chama. Hatua kali zitachukuliwa kwa mwana CCM yeyote atakaye kiuka agizo hili.


Lakini pia ni marufuku kwa viongozi na watendaji wa Chama kujihusisha na kuwakusanyia wapiga kura watu hao wenye nia ya kugombea kupitia CCM kwenye uchaguzi wa dola. Hatua kali zitachukuliwa dhidi ya viongozi na watendaji wote watakao kiuka agizo hili la Chama.


Tunawataka wote wenye nia, viongozi na watendaji wa CCM kuzingatia agizo hili, ili tusije laumiana mbele ya safari.




Imetolewa na;-


Nape Moses Nnauye
Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi
Previous Post Next Post