KOCHA wa Malaga Manuel , amethibitisha kuwa ataihama klabu hiyo baadaye mwaka huu.
Tangazo hilo sasa linatoa fursa kwa kocha huyo kujiunga na klabu ya Manchester City, ambako amekuwa akihusishwa nayo kwa muda mrefu.
Pelegrini anatarajiwa kumrithi Roberto Mancini ambaye alifutwa kazi na Manchester City wiki moja iliyopita.
Kocha huyo alitoa tangazo hilo wakati wa sherehe za kutoa tuzo kwa wachezaji mjini Malaga.
''Siondoki kwa sababu ya fedha, lakini kwa sababu ya mradi fulani wa michezo ambao utanipa fursa nzuri'' Alisema kocha huyo.
Pelegrini mwenye umri wa miaka hamsini na tisa amewahi kuwa kocha wa Villarreal na Real Madrid na aliiongoza klabu ya Malaga kufika robo fainali ya kuwania kombe la klabu bingwa barani ulaya mwaka huu.
Klabu hiyo ya Uhispania ilibanduliwa nje ya mashindano hayo na klabu ya Borussia Dortmund ya Ujerumani ambayo imefuzu kwa fainali ya kombe hilo.
Amesema ataiongoza klabu hiyo katika mechi yake ya mwisho siku ya Jumapili dhidi ya Rosaleda.
Pelegrini aliandikisha historia kwa kuongoza klabu hiyo ya Malaga kufuzu kwa robo fainali ya kombe hilo la Ulaya kwa mara ya kwanza.
Tayari Malaga imefuzu kwa fainali za mwaka ujao baada ya kumaliza katika nafasi ya nne kwenye msururu wa ligi ya La Liga.
Chanzo: bbcswahili