MFAHAMU MKURUGENZI MTENDAJI MPYA WA NBC


nbc 80ab3

Uongozi wa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) umemkaribisha rasmi Mkurugenzi Mtendaji wao mpya, Mama Mizinga Melu. Mama Melu alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Standard Chartered Zambia, ambapo aliongoza benki hiyo kwa Miaka 6 kabla kuhamia NBC.
Mizinga si mgeni kwenye sekta ya kibenki, kwani keshashika nafasi kubwa  mbali mbali akiwa na Benki ya Standard Chartered. Nafasi hizi ni kama vile Mkuu wa Kimataifa wa Mashirika ya Maendeleo, Uingereza ambapo alikuwa anasimamia maendeleo ya mikakati na utekelezaji, pamoja na kuwa Mkuu wa Taasisi za Fedha nchini Kenya na Afrika Kusini, Kanda ya Afrika.
Mama Melu si mgeni kwa Tanzania, kwani alishawahi kuwa Mkuu wa Hazina katika Benki ya Standard Chartered Tanzania kati ya mwaka 2000 na 2003. Kabla ya kushika nafasi hiyo alifanya kazi kama kaimu Mkuu wa Hazina Benki ya Standard Chartered Uganda mwaka 1998 na Zambia mwaka 1999.
Mizinga ana Shahada ya Pili (Masters) ya usimamizi wa Biashara (MBA) kutoka Chuo cha Henley Management College (Uingereza) na ni mwanachama wa Taasisi ya wafanyakazi wa mabenki(ACIB), pamoja na sifa nyengine mbali mbali.
Akizungumzia juu ya uteuzi huo, Mwenyekiti wa  Bodi ya Wakurugenzi ya NBCi, Dk Mussa Assad alisema, “kuwasili Mizinga ni jambo la furaha sana kwetu kwani amekuja wakati muafaka ambapo NBC inapitia mabadiliko mengi mazuri na tunafuraha kuwa atakuwa sehemu ya mabadiliko haya”.



Pia aliongeza” Kabla ya kuwasili kwake, benki ilikuwa ikiongozwa na Pius Tibazarwa ambaye ameonyesha uongozi mzuri kwa kipindi hiki na kutimiza matarajio yetu yote, na tungependa kumshukuru kwa juhudi zake kwani ametekeleza majukumu ya ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji, juu ya jukumu la kuendesha idara yake mwenyewe.”
 Mama Melu amepokea nafasi hiyo kutoka kwa Pius Tibazarwa ambaye alishikilia nafasi hiyo kama Kaimu Mkurugenzi Mtendaji tangu mwanzo wa mwaka huu.
Mizinga amepangiwa kukutana na viongozi wa serikali pamoja na wateja wakubwa kwa ajili kutambulishwa rasmi kabla kuanza safari za kutembelea matawi ya NBC yaliopo mikoani ili kukutana na wafanyakazi na wateja walioko huko. 
Previous Post Next Post