Askari ambaye ni raia wa Pakistan katika kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo,(DRC), ameuawa katika shambulio la kushtukiza.Msafara wa Umoja wa Mataifa ulishambuliwa na watu wasiojulikana mashariki Kusini mwa jimbo la Kivu Jumanne jioni, msemaji wa UN Martin Nesirky amesema.
Katibu Mkuu wa UN, Ban Ki – Moon ameshutumu shambulio hilo akisema mauaji ya askari huyo wa kulinda amani ni uhalifu wa kivita.
Kuna askari wapatao 19,000 wa UN nchini DRC ambako vikundi kadhaa vyenye silaha vinaendesha shughuli zake katika eneo la mashariki lenye utajiri mkubwa wa madini.
Katika taarifa yake, Bw. Nesirky amesema Bwana Ban ameshutumu vikali mauaji hayo na kueleza kuwa yanashtakiwa chini ya sheria za Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC).
Ameongeza kuwa, Katibu Mkuu wa UN ameitaka serikali ya DRC kuwachukulia sheria wahusika wa mauaji hayo. Chanzo: bbcswahili
Mnamo Machi mwaka huu, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipitisha mpango wa kupeleka kikosi cha askari 2,500 mashariki mwa DRC kusimamia amani na kuvinyang’anya silaha vikundi vya waasi.
Mapigano ya hivi karibuni ya kikundi cha waasi cha M23 yalianza mwaka mmoja uliopita Kaskazini mwa mkoa wa Kivu na kusababisha watu wapatao 800,000 kuyakimbia makazi yao.