Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, akiwaonyesha waandishi wa habari, moja ya magari yaliyokamatwa na jeshi hilo. Picha na Zacharia Osanga Dar es Salaam. Polisi katika Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, wamekamata magari manne ya wizi likiwamo moja lililoibwa kutoka nchini Msumbuji. Kamanda wa Polisi wa kanda hiyo, Suleiman Kova alisema magari hayo yamekamatwa katika operesheni ya polisi iliyodumu kwa siku mbili. Kova pia alisema mbali na kukamata magari hayo, polisi pia wamekamata silaha nane zikiwamo bunduki sita na bastola mbili. Pia risasi 27 zilizokuwa zikitumika katika matukio mbalimbali ya uhalifu. Alisema magari yaliyokamatwa ni pamoja Ford Ranger, gari ambalo liliibwa Msumbiji. Mengine ni Mitsubish Canter, Toyota Noah na Toyota Cresta. Kwa mujibu wa kamanda, watuhumiwa watano wamekamatwa wakihusishwa na wizi huo na watafikishwa mahakamani baada ya kukamilika kwa uchunguzi Katika operesheni hiyo iliyohusisha mikoa yote mitatu ya kanda maalumu, ambayo ni Ilala, Kinondoni na Temeke daladala 447 zilikamatwa kwa makosa mbalimbali ya usalama barabarani. Kamanda Kova alisema jumla ya Sh26.5 milioni zilikusanywa kutokana na faini za makosa hayo. Naye Kamanda wa polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela amesema jeshi hilo mkoani kwake linaendelea na operesheni ya kuwasaka wanawake wanaofanya biashara ya ukahaba. Alisema hadi juzi walikuwa wanawashikilia wanawake wanane waliowakamata katika eneo la Uwanja wa Fisi, Tandale, wakijihusisha na biashara hiyo. Tatizo la baadhi ya wanawake kujihusisha na biashara ya kuuza miili yao, imekithiri zaidi katika mitaa ya katikati jijini. Mara kadhaa wanawake wa aina hiyo wamekamatwa na kufikishwa mahakamani, lakini hatua hiyo haijasaidia sana katika kukomesha biashara hiyo. Baadhi ya wanawake waliowahi kuhojiwa kuhusu kiini kinachowasukuma kuuza miili yao bila hata kujali kuambukizwa virusi vya ugonjwa wa Ukimwi, wamedai kuwa hali ngumu ya maisha ndiyo inayowasukuma. Walisema wanafanya hivyo, ili kupata fedha za kuwawezesha kujikimu kimaisha. Baadhi yao wamekiri kutokutumia mipira. |