MENGI AVIONYA VYOMBO VYA HABARI


MWENYEKITI wa Umoja wa Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania (MOAT), Dk. Reginald Mengi, amecharuka na kuvionya vyombo vya habarikuacha kutumika kujenga ajenda zinazohatarisha usalama wa raia na kubomoa amani iliyopo.


Pia amevitaka vyombo hivyo kuacha kutumiwa na wanasiasa mithili ya kondomu na kugeuka kuwa kioo cha wakubwa na wenye fedha badala ya kuwa kioo cha jamii.

Dk. Mengi alitoa onyo hilo jijini Dar es Salaam jana, wakati akifunga mdahalo uliohusu umuhimu wa waandishi wa habari kushiriki kulinda ya amani nchini.

Alisema vyombo vya habari, vinatakiwa kujichunguza kabla ya kuandika na kukuza mambo yanayohatarisha usalama wa nchi.

"Nchi yetu imejaliwa kuwa rasilimali nyingi sana, lakini amani




inapotoweka ina hatarisha usalama wa kila mwananchi, hakuna atakayepona, jambo la msingi tuache kulalamika tuchukue hatua.

"Tunapozungumza chanzo cha uvunjifu wa amani kwa mfano suala la vurugu za kidini kuhusu kugombania kuchinja, ni suala ambalo tunaweza kukuta lililetwa na mtu ambaye hata hayupo nchini, hapa tunahitaji kufanya uchunguzi wa suala hili tusipende kushupalia vitu ambavyo tunaona kabisa vinaweza kubomoa amani iliyopo.

"Hivi sasa vyombo vya habari, vimeanza kumeguka na kutumiwa na wakubwa na wenye nazo, hii ni hali ya hatari sana kwa nchi yetu, kwa sababu badala ya kuandika habari za wanyonge sasa zimebakia kuwandikwa habari za wakubwa pekee.

"Tunapaswa kuwa wazalendo... tukumbuke kuwa hawa watu wanalenga kuwatumia wandishi wa habari kama vile kondom, akishakutumia basi anakutupa," alisema.

Previous Post Next Post