KOCHA TUKUYU STARS “BANYAMBALA” APONDA MFUMO WA SOKA LA VIJANA!

Na Baraka Mpenja wa fullshangwe-Dar es Salaam.

…………………………………………………………..

Kocha mkuu wa mabingwa wa zamani wa kandanda nchini Tanzania mwaka 1986 , klabu ya Tukuyu Stars “Banyambala”, na aliyekuwa kocha mkuu wa timu ya vijana ya mkoa wa Mbeya iliyoshiriki Copa Coca Cola 2011, Chuma Edson Amos amesema kupotea kwa klabu hiyo katika soka la ushindani nchini Tanzania kumechangia kushuka kwa soka la mkoa wa Mbeya.

Akizungumza na mtandao huu, Chuma aliyewaongoza “Banyambala” na viatu vyao miaka ya 2011-2004 kabla ya kushuka daraja alisema, klabu hiyo ilikuwa kitalu cha kuzalisha wachezaji vijana hivyo kupotea kwake kumeligharimu soka la mkoa huo hasa maafande wa kupiga gwaride Tanzania Prisons wanaowakilisha mkoa wa Mbeya ligi kuu soka Tanzania bara msimu huu.

Chuma alisema kihistoria wachezaji wengi waliotamba na Prisons ya ukweli wakiwemo Geofrey Bony, Shadrack John Nsajigwa, Ivo Mapunda na wengine wengi, chimbuka lao lilikuwa Tukuyu stars ambayo kwa sasa inajivutavuta kurejea soka la ushindani kufuatia mkuu wa wilaya ya Rungwe Chrispin Meela kuanzsisha mpango wa kuifufua timu hiyo mwaka jana.

“Unajua Tukuyu Stars tulipika vijana wengi sana kutoka ndani ya jiji la mbeya, tulikuwa tunachukua wachezaji wachache kutoka mikoa jirani ya Iringa, Ruvuma na Rukwa, lakini tuliangalia zaidi nyumbani, na ndio maana tulifanikiwa kupata vijana wengi wenye vipaji wakitawaliwa na nidhamu kubwa ya soka”. Alisema Chuma.

Chuma alilisisitiza kuwa kitendo cha viongozi wa timu ya Prisons na chama cha soka mkoani Mbeya kushindwa kuwekeza kwenye soka la vijana kwa kuanzisha mashindano mbalimbali baada ya michuano ya kitaifa ya Copa Coca Cola ndio chimbuko la timu hiyo kuhangaika huku na kule iking`ang`ana kukwepa rungu la kushuka daraja msimu huu.

“Vijana wakitoka Coca Cola wanaachwa kama yatima, badala ya kuwaendeleza kwa pamoja ili waimarike zaidi kimichezo wanatupwa tu, mfumo huu umeliweka rehani soka la Mbeya tofauti na miaka ya nyuma”. Alisisitiza Chuma.

Mbali na kuongelea soka la vijana jijini Mbeya, pia alitupia jicho la tatu soka la vijana la Tanzania na mfumo wake.

Kocha huyo aliwataka viongozi wa shirikisho la soka Tanzania TFF kuacha kasumba ya kujaza vijana wa mikoa mikubwa hasa Dar es salaam kwenye timu za taifa za Tanzania.

Chuma aliongeza kuwa wachezaji wengi wanaotamba katika soka la Tanzania kama Juma Kaseja, Jerryson Tegete na wengineo, asili yao ni mikoani, kitu ambacho kinamaanisha vipaji vipo zaidi ya Dar es salaam.

“Nakumbuka Serengeti Boys iliweka kambi jijini Mbeya kwa muda wa wiki mbili, ilicheza mechi za kirafiki, lakini cha kushangaza viongozi wa timu hawakuona hata mchezaji yeyote wakuongezwa kikosini siku za usoni, hakika ni jambo la ajabu sana”. Alisema Chuma.

Aidha kocha huyo aliwataka viongozi wa soka kusoma alama za wakati kwani dunia nzima sasa inawekeza katika soka la vijana.

Alisema ni wakati wa kujenga vituo vya soka maeneo mbalimbali hasa mikoani pamoja na kuwaendeleza vijana kwa kuanzisha mashindano mbalimbali mikoani na kitaifa.
Previous Post Next Post