KENYA YAIMWAGIA SIFA KEMKEM KAMPUNI YA MCDONALD LIVE LINE TECHNOLOGY YA TANZANIA






 Mmiliki wa Kampuni ya McDonald Live Line Technology, McDonald Mwakamele (kulia) akiwaonesha maofisa kutoka Kampuni ya Umeme ya Kenya (KPCL), vifaa mbalimbali vinavyotumika kutengeneza umeme bila kuuzima walipotembelea chuo cha kampuni hiyo, mwanzoni mwa wiki, wilayani Mvomero, Morogoro. Kenya iko mbioni kuingia mkataba na kampuni hiyo kwa ajili ya mafundi wao kufundishwa teknolojia hiyo ya kisasa. Kutoka kushoto ni maofisa wa KPCL, Meneja Uendeshaji, Noah Ogano, Peter Waweru na Mhandisi Charles Mwaura ambaye ni Naibu Meneja Huduma za Kawaida.
 Mwakamele akiwaonesha maofisa wa KPCL, baadhi ya vifaa vinavyotumika katika kazi hiyo. 
 Mwakamele akiwaonesha maofisa wa KPCL kifaa kinachotumika kubebea nguzo.
 Mwakamele akiwaonesha gari maalumu linalotumika kumpeleka fundi kutengeneza nyaya na vikombe juu ya nguzo.
 Mwakamele akionesha jinsi ya kutengeneza vikombe vya umeme
 Mwakamele akiwa juu ya nguzo akionesha jinsi ya kutengeneza umeme bila kuukata.
 Naibu Meneja wa KPCL, Mhandisi Charles Mwaura akikabidhiwa na Mwakamele mavazi maalumu ya kazi yasiyopisha umeme.
 Mhandisi Mwaura wa KPCL, akivishwa na Mwakamele moja ya mavazi hayo
Mhandisi Mwaura akimshukuru Mwakamele




Na Mwandishi Wetu, Morogoro

UONGOZI wa Shirika la Umeme nchini Kenya(KPLC), umesema kuwa unaangalia namna ya kuingia makubaliano ya wataalamu wake kuja nchini Tanzania ili kujifunza kutumia teknolojia ya kufanya matengenezo ya umeme bila kuukata.
 
Uamuzi huo unatokana na kile ambacho uongozi huo umeeleza wananchi wa Kenya wamechoshwa na tabia ya kukatiwa umeme wakati yanapofanyika matengenezo wakati wa kubadili nguzo au vikombe  na sasa wameamua kutafuta dawa ya tatizo hilo.

Wakizungumzia wiki hii mkoani Morogoro walipotembelea kampuni pekee Afrika Mashariki na Kati inayoweza kutengeneza umeme bila kuukata ya McDonald Liveline Technology, walisema wamefurahishwa na teknolojia hiyo na imebaki kwao kuamua ni wataalamu wangapi wajifunze kwa maslahi ya nchi yao.
Walisema kuwa wamefika mkoani hapa kwa sababu tu ya kuridhishwa na utendaji kazi wa kampuni ya McDonald Liveline Technology na kwamba wakiwa nchi jirani wana haki ya kupata utaalamu huo na ndio maana wamefunga safari ili kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo Donald Mwakamele.
Akizungumza zaidi akiwa katika eneo ambalo Kampuni ya McDonald imefunga mitambo yake kwa ajili ya kutoa mafunzo 'Liveline' Meneja wa Operesheni na Huduma wa KPLC Noah Omondi, alisema kuwa Tanzania imepata bahati ya kuwa na mtaalamu huyo na wao watamtumia kwa ajili ya kufanikisha malengo ya nchi yao ya kutokata umeme ovyo wakati wa matengenezo.
Omondi aliyekuwa ameambatana na Mwalimu wa matengenezo ya mtandao wa ugavi wa umeme Peter Waweru na Meneja msaidizi wa huduma na matengenezo wa mkoa wa Nairobi Charles Mwaura alisema kuwa kikubwa ambacho wao wanakitazama sasa ni kutafuta ufumbuzi wa umeme nchini mwao na kwamba hawatarudi nyuma.
Akizungumza zaidi kuhusu kampuni yake Mwakamele alisema teknolojia hiyo ni muhimu kwa nchi mbalimbali na kwamba kuifahamu kwake teknolojia hiyo ameweza kufanya kazi katika mataifa makubwa duniani ikiwemo Marekani na nchi nyingine za Afrika.

Alisema hakuna sababu ya kukata umeme wakati unapoamua kutengeneza kwani teknolojia ambayo inaweza kutumika kufanya matengenezo bila kukata umeme ipo na kwake inapatikana muda wote.

Aliongeza kukata umeme wakati wa matengenezo ni kusababisha hasara ambayo inaweza kuepukika kwa kutumia teknolojia ambayo yeye anaifahamu na anaifundisha.
"Hakuna sababu ya kukata umeme,  njia mbadala ipo ambayo unaweza kuitumia kwa kufanya matengenezo bila kuukata.Tunaifanya teknolojia hii katika nchi mbalimbali.Nipo tayari kuifanya popote na wakati wowote ninapohitajika,"alisema Mwakamele.
Alisisitiza endapo teknolojia hiyo ya matengenezo bila kukata umeme itatumika, Tanzania itaweza kuokoa fedha na muda ambavyo vimekuwa vikipotea kila umeme unapokatwa kwa ajili ya matengenezo kama ya kubadilisha nguzo au kukata miti iliyo karibu na nyaya za umeme.

Hata hivyo alisema anaguswa na uzalendo wa nchi yake, na ndio maana kila mara amekuwa akiwataka watalaamu wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), kufika chuoni kwake kujifunza teknolojia hiyo ambayo ni muhimu katika kipindi hiki kwa maslahi ya taifa.
Previous Post Next Post