JAJI WARIOBA: TUTATOA RASIMU YA KATIBA YENYE MASLAHI YA TAIFA





Tume ya Mabadiliko ya Katiba imesema imejipanga kuandaa rasimu ya katiba itakayoweka mbele maslahi ya taifa na kuwaomba wananchi waijadili na kutoa maoni yao katika mabaraza ya katiba yatakayokutana kuanzia mwezi Juni mwaka huu (2013). 
 Mwenyekiti wa Tume hiyo Jaji Jospeh Warioba amesema leo (Jumatatu, Aprili 29, 2013) jijini Dar es Salaam kuwa katika kuandaa rasimu hiyo, Tume yake haitapokea shinikizo kutoka taasisi, asasi, makundi au vyama vya siasa.
 “Tume haitengenezi katiba ya vikundi au vyama, tunaandaa katiba ya nchi,” amesema Jaji Warioba katika mkutano wake na waandishi wa habari katika ofisi za Tume.
Amefafanua kuwa Tume inazingatia uzito wa hoja zilizotolewa na wananchi na sio idadi ya watu waliotoa maoni. Jaji Warioba amewataka wananchi kutokubali kutumiwa na makundi, asasi, taasisi na vyama wakati wa kujadili na kutoa maoni katika mabaraza ya katiba ya wilaya.

Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji Joseph Warioba akiongea na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo (Jumatatu, Aprili 29, 2013). Kulia ni Katibu wa Tume, Bw. Assaa Rashid.

Mwenyekiti wa kamati ya uwasilishaji wa mapendekezo ya muundo wa mabaraza ya Katiba kwa jamii ya watu wenye ulemavu, Bw. David Nyendo (kushoto) akiwasilisha maoni yake ya kamati hiyo kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba katika mkutano baina yao uliofanyika  ofisi za Tume Jijini Dar es Salaam tarehe 13 Feb mwaka huu (2013). Kulia ni Mjumbe wa Tume, Dkt. Salim Ahmed Salim. (Picha na Tume ya Katiba)

Previous Post Next Post