Nahodha wa watukutu wa London, klabu ya Tottenham Hospur, Michael Dawson amesema timu yake inaweza kufanya maajabu na kuwafumua wapinzani wao Basel ya Uswisi mchezo wa ligi ya Uropa unaotarajia kupigwa usiku wa leo katika dimba la mtakatifu Jakob-park na hatimaye kufuzu hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo.
Nyota huyo amesema kuwa kuna watu wanafikiri kuwa matokeo ya sare ya 2-2 wiki mbili zilizopita jijini London yamewaathiri sana na hawana uwezo wa kuyapindua, lakini wao wanajiamini na wanaweza kushinda na kuwaduwaza mashabiki wataofurika uwanjani leo.
Nyota huyo amewaondoa hofu na kuwajengea imani ya ushindi mashabiki wa klabu hiyo ambayo katika dimba lake la nyumbani la White Hart Lane walianzia nyuma na kusawazisha mabao mawili baada ya kufungwa mapema.
Akizungumzia mkakati wake wa kubakia klabuni hapo katika dirisha dogo la usajili, Dawson, amesema ataendelea kupambana kubakia ingawa kocha wake Andre Villas-Boas AVB ameonesha nia ya kumuuza katika klabu ya QPR majira ya joto.
Nyota huyo ambaye amepata namba katika kikosi cha kwanza baada ya Younes Kaboul kukumbwa na majeruhi amesema bado anaamini kuwa ataisaidia timu na kufikia mafanikio makubwa.
“Ningekuwa nimeshaondoka Spurs, lakini kamwe sikati tamaa, leo hii ni furaha kubwa kwang kuwaongoza vijana na nitajisikia faraja sana endapo tutafanikiwa, najua haitakuwa kazi nyepesi lakini lazima mtu uwe na imani”. Amesema Dawson.
Spurs itamkosa mpachika mabao wake Gareth Bale ambaye ni majeruhi, lakini wanamtegemea sana Mtogo Emmanuel Adebayor ambaye AVB anaamini atawaongozwa vyema mbele ya Basel.