TAARIFA ZA KIMICHEZO KUTOKA TFF IKIWEMO PONGEZI KWA TIMU YA AZAM FC KUWA KUSHINDA UKO LIBERIA.


Boniface Wambura.
Ofisa Habari Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
 HONGERA AZAM KWA USHINDI LIBERIA
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linaipongeza klabu ya Azam kwa ushindi wa mabao 2-1 ilioupata timu yake katika mechi ya raundi ya kwanza ya michuano ya Kombe la Shirikisho.
Mechi hiyo dhidi ya Barrack Young Controllers II ilichezwa jana jijini Monrovia, na timu hizo zitarudiana wikiendi ya Aprili 6 au 7 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. 
Ushindi huo unaiweka Azam chini ya kocha wake Stewart John Hall katika mazingira mazuri ya kusonga mbele baada ya mechi ya marudiano. Bila shaka ushindi wa timu ya Azam pamoja na mambo mengine umechangiwa na klabu hiyo kujipanga vizuri.
Hata hivyo ushindi huo bado ni changamoto kwa wachezaji, benchi la ufundi na uongozi wa Azam kuhakikisha unajipanga vizuri kwa mechi ya marudiano kwa vile mpira wa miguu una matokeo ya aina tatu; kushinda, kutoka sare au kufungwa.
Msafara wa timu ya Azam unaoongozwa na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF, Blassy Kiondo unatarajiwa kurejea nchini kesho alfajiri kwa ndege ya Kenya Airways kupitia Nairobi.
TAIFA STARS TRAINING PROGRAMME
Taifa Stars itacheza mechi ya mchujo kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Dunia mwaka nchini Brazil dhidi ya Morocco. Mechi hiyo itachezwa Jumapili katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Jumamosi, Machi 16- Wachezaji kuanza kuripoti kambini
Jumapili, Machi 17- Mazoezi Uwanja wa Karume- Saa 2 asubuhi
Jumatatu, Machi 18- Mazoezi Uwanja wa Karume- Saa 9 alasiri
Jumanne, Machi 19- Mazoezi Uwanja wa Taifa- Saa 9 alasiri
Jumatano, Machi 20- Mazoezi Uwanja wa Taifa- Saa 2 asub na saa 9 alasiri
Alhamisi, Machi 21- Mazoezi Uwanja wa Taifa- Saa 9 alasiri
Ijumaa, Machi 22- Mazoezi Uwanja wa Taifa- Saa 9 alasiri
Jumamosi, Machi 23- Mazoezi Uwanja wa Taifa- Saa 10.30 jioni
PONGEZI KWA UONGOZI MPYA TAFCA
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linatoa pongezi kwa uongozi mpya wa Chama cha Makocha wa Mpira wa Miguu Tanzania (TAFCA) uliochaguliwa katika uchaguzi uliofanyika juzi (Machi 16 mwaka huu) mjini Dodoma.
Ushindi waliopata viongozi waliochaguliwa kuongoza chama hicho unaonesha jinsi wajumbe wa Mkutano Mkuu wa TAFCA walivyo na imani kubwa kwao katika kusimamia taaluma ya ukocha nchini.
TFF inaahidi kuendeleza ushirikiano wake kwa Kamati ya Utendaji ya TAFCA chini ya uenyekiti wa Oscar Don Koroso aliyeibuka mshindi kwa kura zote za ndiyo baada ya kukosa mpinzani.
Uongozi huo mpya una changamoto nyingi, kubwa ikiwa ni kuhakikisha unaendesha shughuli za mpira wa miguu kwa kuzingatia katiba ya TAFCA pamoja na vyombo vya mpira wa miguu vilivyo juu yake.
Pia tunatoa pongezi kwa Kamati ya Uchaguzi ya TAFCA chini ya Ramadhan Mambosasa na Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa kuhakikisha uchaguzi huo unaendeshwa kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF.
Safu nzima ya uongozi wa TAFCA iliyochaguliwa inaundwa na Dk. Oscar Dan Koroso (Mwenyekiti), Lister Manyara (Makamu Mwenyekiti), Michael Bundala (Katibu Mkuu), Gabriel Gunda (Katibu Msaidizi), Dismas Haonga (Mhazini), Wilfred Kidao (mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF).
Wajumbe wa Kamati ya Utendaji waliochaguliwa ni Jemedari Saidi, George Komba na Magoma Rugora.
 

Previous Post Next Post