MEYA WA ILALA AKAGUA MAENDELEO YA UJENZI WA BARABARA YA MOROGORO YA MAGARI YAENDAYO KWA KASI.



Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilala Jerry Silaa akijadili na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usafiri wa Haraka (DART) Asteria Mlambo pamoja na watendaji wengine umuhimu wa kufanyika mkutano wa pamoja ili kuweza kutatua changamoto zinazojitokeza wakati ziara yake ya kukagua ujenzi wa barabara ya magari yaendayo kwa kasi katika barabara ya Morogoro hadi Sokoine.






Picha juu na chini ni Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usafiri wa Haraka (DART) Asteria Mlambo (aliyenyoosha mkono) akifafanua jambo kwa Mstahiki Meya wakati wa ukaguzi wa barabara hiyo.





Muonekano wa Barabara ya Morogoro ambayo bado inayoendelea kukarabatiwa kwa ajili ya magari yaendayo kwa kasi ambayo imekuwa kikwazo kwa wafanyabiashara na pia sasa imegeuka kuwa njia maarufu ya Bodaboda zinazoendeshwa kwa kasi na kuwa hatari kwa watembea kwa miguu ambao wamekuwa wakigongwa katika barabara hiyo.



Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilala Mh. Jerry Silaa akizungumzia changamoto zinazojitokeza kufuatia ujenzi wa barabara ya Morogoro ambapo limejitokeza suala la wafanyabiashara kuona kwamba itakapo kamilika magari madogo yatakuwa hayapiti tena barabara hiyo hivyo hawajui hatma ya biashara zao haswa kuanzia Bibi Titi hadi Sokoine na kusema iko haja ya kukaa na wafanyabiashara hao kuwaeleza kuwa maendeleo hayakwepeki.

Akijibu baadhi ya kero na maswali ya wakazi wa jiji kuhusu kucheleweshwa na kuvurugwa kwa taratibu za barabara hiyo, Mstahiki meya amesema hiyo inatokana na watu haswa wafanyabisha kujijengea miundo mbinu bila kufuata taratibu za jiji, kitu ambacho kimesababisha mkandarasi anapofanya kazi yake anakutana na mitaro, bomba za maji safi na taka, mikongo ya mawasiliano ambazo haziko kwenye ramani na hapo lazima awatafute wahusika nao wanataratibu zao hivyo kuwa kikwazo kwake kukamilisha ujenzi huo.



Mmoja wa wafanyabiashara wa eneo hilo Andrew John Shayo akielezea malalamiko yao kuwa tangu ujenzi wa barabara hiyo uanze biashara hazifanyiki kwa kuwa magari madogo hayapiti pia kumekuwa na tatizo la kupatikana kwa maji kutokana na mkandarasi huyo kukatakata mabomba ya DAWASCO na kuwa pindi mvua zinaponyesha maji yamekuwa hayaendi na kusababisha madimbwi na kushauri ukarabati huo uharakishwe kwa kuwa wao ndio waathirika wakubwa wa ujenzi huo.



Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usafiri wa Haraka (DART) Asteria Mlambo akifafanua kuwa mradi huo una mafungu saba ya utekelezaji na kati ya hayo fungu la saba lilishakamilishwa ambalo ni uhamishaji wa nyaya za Umeme lakini Kandarasi kuu tuliyonayo sasa hivi ambayo inawagusa watu wengi wa Dar es Salaam ni ujenzi wa miundo mbinu ya barabara, na kuwataka watu kuwa wavumilivu kwa kuwa mkandarasi anashughulikia kwanza barabara kutoka Kimara hadi Kivukoni.



Picha Juu na chini ni Mstahiki Meya Jerry Silaa akiwa katika eneo lenye dimbwi la maji ameshauri Ili kupunguza msongamano tunafanya utaratibu angalao sasa tufungue barabara za India, jamhuri, Libya ili angalao kupunguza msongamano wa upande mmoja wa mji lakini baadae itabidi kujadiliana ili ujenzi huu ukikamilika mwezi Juni kutakuwa na changamoto za aina gani kwa pamoja na viongozi wa mitaa, wafanya biashara, wenzetu wa DART ili tuone biashara za watu zitaendelea kwa staili ya aina gani.

Amesema hatuwezi kubaki na jiji lilelile la zamani lazima tubadilike, kwa mradi wa kisasa kama huu Tanzania kwa maana ya jiji la Dar es Salaam ndio litakuwa la pili barani Afrika, mradi kama huu mpaka sasa uko Afrika Kusini peke. Na hizi barabara zinajengwa kwa kiwango cha zege hivyo zinadumu kwa miaka mingi.



Na.Mwandishi wetu

Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala Jerry Silaa ameitisha mkutano wa pamoja na wafanyabiasha, wadau na watendaji wa idara mbalimbali za serikali ili kujadili changamoto zinazojitokeza wakati wa utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa barabara ya mabasi yaendayo kasi (DART).

Mstahiki Silaa amefikia uamuzi huo baada ya kujionea changamoto mbalimbali zinazojitokeza wakati wa mradi huo katika makutano ya barabara za Bibi Titi na Morogoro hadi barabara ya Sokoine ambazo zimekuwa kero kubwa kwa wafanyabiashara na wakazi wa maeneo hayo.

Akizungumza baada ya kufanya ziara ya mradi huo katika barabara hizo, Silaa amesema kuna haja ya kuwepo kwa mkutano wa wadau mbalimbali kutoka Shirika la Nyumba (NHC), Mamlaka ya Maji Dar es Salaam (DAWASCO), Mamlaka ya Mapato Nchini (TRA) na wafanyabiashara katika maeneo ya mradi huo ili kujadili na kufikia muafaka wa pamoja wa kutatua changamoto hizo.

Meya huyo amesema changamoto ni nyingi lakini zinaweza kutatuliwa ikiwa wadau wote wanaohusika katika mradi huu watakutana na kujadili kwa kina njia na hatua stahiki za kukabiliana na changamoto hizo.

Amezitaja changamoto ambazo zinajitokeza wakati wa mradi huo kuwa ni pamoja na kuongezeka kwa foleni baada ya njia nyingi kufungwa, kukosekana mahala pa kuegesha magari, kutokuwepo na njia za kupitisha magari ya zima moto na uharibifu wa miundombinu ya maji wakati wa ujenzi wa barabara.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usafiri wa Haraka (DART), Asteria Mlambo amesema kuwa pamoja na changamoto hizo zinazojitokeza wakati wa utekelezaji wa mradi lakini jitihada za makusudi zinafanyika kuzitatua hasa zile zilizo ndani ya uwezo wetu.

Amesema mwenendo wa mradi huo unakwenda katika malengo yaliyopangwa kulingana na makubaliano ya mkandarasi wa mradi huo Strabag ili kutekeleza ahadi yake kwa Serikali ya kukamilisha mradi huo hadi ifikapo mwaka 2015.

Ameongeza kuwa utekelezaji wa mradi huu unaendelea vizuri pamoja na changamoto za hapa na pale, tunaomba ushirikiano wa wananchi na watumiaji wa barabara kwa ujumla kuheshimu na kufuata maelekezo ya barabarani yanayowakataza kutumia barabara zilizo kwenye matengenezo.
Previous Post Next Post