
Katibu Mkuu wa CCM Abdulrahman Kinana (wapili kushoto) na ujumbe wake, wakionyweshwa maumbo ya namna kiwanda cha viatu cha Huajian mjini Dongguan, China, alipotembelea kiwanda hicho, Machi 13, 2013, akiwa katika ziara ya mafunzo, nchini China. (Picha na Bashir Nkoromo).
NA: BASHIR NKOROMO, CHENGDU, CHINA
KATIBU Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana amesema, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kitaihimiza serikali yake, kuiga mbinu zinazotumiwa na Chama Cha Kikomunisti cha China (CPC) ya kuweka vituo vya vijana wajasiriamali wasomi, kuwezesha wanaomaliza elimu ya juu waweze kutumia vipaji vyao kujiajiri badala ya kusubiri kuajiriwa.
Tanzania ikifanikiwa kufanya hivyo, itajikomboa kwa kuwasaidia vijana wengi ambao baada ya kumaliza masomo huhangaika kutafuta kazi za kuajiriwa badala ya kijiajiri wenyewe kutokana na elimu, ujunzi na ubunifu walio nao.
Kinana alisema, hayo leo Machi 14, 2013 baada yeye na ujumbe wake wa watu 14, waliopo katika ziara ya siku kumi ya mafunzo nchini China, kutembelea Kituo cha vijana wajasiriamali cha Chengdu, jimbo la Sichuan na kushuhudia jinsi vijana wasomi walivyoweza kutumia vipaji vyao kujiajiri baada ya kukusanywa kwenye kituo hicho kinachoitwa, Chengdu Hich Tech Postgraduetes Enterpreneurial Park.
“Kwa kweli vijana hawa wanaonyesha umahiri mkubwa wa kutumia vipaji vyao, ni muhimu nasi tukaiga namna hii bora ya kuwaweka vijana pamoja, kwa sababu inasaidia kupunguza tatizo la ajira na pia kuleta faida kwa taifa”, alisema Kinana.
Kinana alimwagiza Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Martine Shigela aliyeko kwenye msafara wake, kuwasiliana na uongozi wa kituo hicho ili kuona namna mbinu zinazotumika kuwakusanya vijana kwenye kituo hicho zitakavyoweza kufanyika Tanzania.