RAISI JAKAYA KIKWETE KUTAJA KAMATI KUU


MWENYEKITI wa CCM Taifa, Rais Jakaya Kikwete anatembea na mkoba wenye majina ya wajumbe wapya wa Kamati Kuu (CC) ya CCM hadi hapo atakapowatangaza kesho kutwa hivyo kuwaacha wajumbe wengi wa Halmashauri Kuu (NEC) wa chama hicho wakiwa roho juu iwapo majina yao ni miongoni mwake au l
Baadhi ya wajumbe hao walionekana jana katika viunga vya ofisi za makao makuu ya chama hicho (White House) mjini hapa wakiomba kura kwa wajumbe wenzao kama majina yao yatakuwa kwenye orodha hiyo ya Rais Kikwete...

“Nawaombeni mnikumbuke jina langu likija,” alisema mmoja wa wajumbe wa NEC ambaye pia ni Waziri wa Serikali ya awamu ya nne ambaye jina lake tunalihifadhi kwa sababu za kimaadili.
Ingawa baadhi ya wajumbe walimkejeli, wapo waliomtia moyo wakimwambia: “wewe bwana una akili sana, umekifanyia Chama kazi nyingi sana. Lazima jina lako lirudi.”
Wajumbe wa CC walipaswa kuteuliwa kwenye NEC iliyofanyika Novemba 10 hadi 12, mwaka jana lakini Rais Kikwete alisitisha mpango huo kwa kile alichosema kuwa anahitaji muda zaidi ili awafahamu vyema wajumbe wa NEC mpya iliyoteuliwa wakati huo.
Hali hiyo imekuwa ikiwaweka roho juu wajumbe wa NEC kwa kuwa wengi wao na hasa waliokuwa kwenye CC iliyopita wanatamani kuteuliwa tena.
Kutokana na subira hiyo ya Rais Kikwete, Chama hicho tawala kilisheherekea kutimiza umri wa miaka 36, Jumanne iliyopita mjini Kigoma, bila ya kuwa na Kamati Kuu, ambayo ilitakiwa kukaa na kutathmini mafanikio na matatizo ya chama hicho.
Jana, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema kuwa NEC itafanya kikao kwa siku mbili kuanzia kesho kutwa chini ya Uenyekiti wake Rais Jakaya Kikwete.
Kwa mujibu wa Nnauye, pamoja na mambo mengine kikao hicho kitatanguliwa na semina ya siku mbili kwa wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa.“
Lengo la semina hii ni kuwaongezea wajumbe uelewa kuhusu masuala ya chama hicho na Serikali yake hasa ikizingatiwa kwamba wengi wa wajumbe ni wapya kutokana na wengi kuchaguliwa kwenye uchaguzi mkuu wa chama mwaka jana,” alisema.
Nnauye alisema kuwa semina hiyo itakuwa na mada kuu nne ambazo ni pamoja na ‘Nafasi ya wajibu wa mjumbe wa Halmashauri Kuu Taifa’, ‘Umuhimu wa maadili kwa viongozi na watendaji wa chama hicho’, ‘Mikakati ya kutekeleza maazimio ya Mkutano Mkuu wa Taifa wa nane wa CCM’ pamoja na ‘Mkakati wa kukuza ajira nchini’.
“Semina hii itafuatiwa na Mkutano rasmi wa Halmashauri Kuu ya Taifa ambao pamoja na mambo mengine uchaguzi wa wajumbe wa Kamati Kuu ya Chama,” aliongeza Nnauye.
Gazeti Mwananchi
Previous Post Next Post