IGP Said Mwema
WAKATI kukiwa na taarifa kwamba maofisa wa Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI) wametua nchini kwa ajili ya kufanya upelelezi wa mauaji ya Padri Evarist Mushi, Jeshi la Polisi limetangaza dau la Sh10 milioni kwa atakayefichua aliyemuua padri huyo.Padri Mushi aliuawa kwa
kupigwa risasi Jumapili iliyopita wakati akienda kuongoza ibada katika Kanisa la Mtakatifu Teresia lililopo Beit el Ras nje kidogo ya mji wa Zanzibar, ambapo inadaiwa kuwa waliomuua walikuwa wamepanda pikipiki aina ya Vespa na walimfyatulia padri huyo risasi tatu akiwa ndani la gari yake.
Wakati polisi wakitangaza dau hilo, Sheikh Ali Khamis Ali (65) mkazi wa Kitope Kaskazini Unguja, aliuawa jana kwa kukatwa mapanga mjini Zanzibar, baada ya wezi kuvamia shambani kwake.
Habari za kuaminika zilizopatikana juzi zinaeleza kuwa maofisa hao wa FBI, wako nchini na tayari na wamekutana na baadhi ya viongozi wa Serikali kwa ajili ya kuanza kazi hiyo.
Chanzo chetu cha habari kimeeleza kuwa maofisa hao walikutana na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi kwa ajili ya kuangalia ni namna gani watafanya shughuli zao katika upelelezi huo.
Pamoja na ushiriki FBI, taarifa zinaeleza kuwa maofisa wa Serikali ya Tanzania wamezungumza na taasisi za upelelezi za nchi tano, ili kuongeza nguvu katika upelelezi huo.
Taasisi nyingine inayotajwa kuwa huenda ikashiriki katika uchunguzi huo ni Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai ya Uingereza (Scotland Yard).
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Pereira Ame Silima alilithibitishia gazeti hili kwamba Serikali imeanza kufanya mazungumzo na mashirika mbalimbali ya upelelezi duniani kwa ajili ya kushirikiana nayo kuchunguza mauaji ya Padri Mushi, lakini akasema kuwa ni mapema mno kuyataja.
“Tumefuata maagizo aliyotoa Rais Kikwete kwamba tushirikishe mataifa mbalimbali kuchunguza mauaji yaliyotokea Zanzibar, siwezi kutaja kwa majina, ila tayari tumeanza kuzungumza na nchi mbalimbali,” alisema Silima.
Akizungumza mjini Zanzibar jana, Kamishna wa Polisi visiwani humo, Mussa Ali Mussa alisema kuwa hadi sasa hakuna mtu aliyefikishwa mahakamani kuhusiana na tukio hilo la mauaji.
“Hakuna aliyefikishwa mahakamani, lakini wapo watu ambao wamekamatwa wakihusishwa na tukio hili na tunaendelea kuwahoji, wengine tunawaachia,” alisema na kuongeza:
“Tumeahidi kutoa Sh10 milioni kwa mtu yeyote, atakayetoa taarifa za mauaji ya Padri Mushi, hii itakuwa kama zawadi tu.”