MKUU MKOA WA KIGOMA MACHIBYA AWATAKATA VIJANA WA JKT KUWA WAZALENDO


E80A2616
Mkuu wa mkoa Kigoma Issa Machibya akizungumza katika hafla ya kufunga mafunzo ya kujitoilea ya jeshi la kujenga taifa kambi ya JKT Kanembwa wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma .MKUU wa mkoa Kigoma Issa Machibya amewataka vijana wanaomaliza mafunzo ya kujitolea ya jeshi la kujenga taifa mkoani humo kutumia mafunzo hayo kama chachu ya kuchochea uzalendo na uwajibikaji kwa vijana wenzao.


 Akizungumza wakati wa hafla ya kufunga mafunzo Operesheni senza katika kambi ya JKT Kanembwa Kikosi cha 824 wilayani Kibondo alisema kuwa vijana hao wanapaswa kufanya kazi popote watakapokuwa kwa mujibu wa kiapo walichokula wakati wakimaliza mafunzo hayo.
 Machibya alisema kuwa kusimamishwa kwa muda kwa mafunzo ya jeshi la kujenga taifa kuliwafanya vijana wengi walioanza utumishi wenzao kufanya kazi kwa mazoea wakiwa hawajajengwa kufanya kazi kizalendo na kujitolea zaidi.
 Mkuu huyo wa mkoa aliwaambia vijana hao wanapaswa kuonyesha kwa vitendo tofauti ilyopo kati yao na vijana wenzao wa mtaani ambao hawajapitia mafunzo hayo na kuonyesha umuhimu wa kuwepo kwa mafunzo hayo..
 Alisema kuwa moja ya mambo hayo ni pamoja na vijana hao kutafuta namna ya kuweza kujiajiri kwa kuanzisha miradi ya kujiingizia kipato na kuwaajiri vijana wenzao wa mtaani kutokana na mafunzo waliyopata badala ya kupiga makelele ya kutaka ajira kutoka serikaliki.
 “Mafunzo ya JKT si tu yanafundisha ukakamavu, lakini pia yanafundisha vijan kazi za ufundi, ujasiliamali mambo ambayo yatawawezesha kuishi maisha ya kujitegemea, kuanzisha miradi ya kiuchumi na vijana wenzao kujifunza kwao namna ya kuendesha maisha kwa kujitegemea badala ya kutegemea ajira ya serikali, hiyo ni fursa mliyopewa kuonyesha tofauti kati yenu mliopata mafunzo na ambao hawakupata mafunzo,” alisema Mkuu wa mkoa kigoma.
 Kwa upande wake Kamanda wa kikosi cha 824 JKT Kanembwa, Erasmus Bugogwe alisema kuwa jumla ya vijana 521 wanamaliza mafunzo hayo ya awali ambapo wameweza kujifunza ukakamavu, medani za kivita na ujasiliamali.
 Alisema kuwa pamoja na hilo vijana hao wameweza kushiriki katika shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo kilimo kwa kuzalisha mbegu kwenye shamba la hekta 35 na kutoa damu kwa ajili ya akiba ya benki ya damu kanda ya magharibi.
 Awali vijana wanaomaliza mafunzo hayo wameishukuru serikali kwa kupata nafasi ya kujiunga na kushiriki mafunzo hayo ambapo hata hivyo wameomba kupewa kipaumbele katika upatikanaji wa ajira zinazotolewa na majeshi na vyombo vya ulinzi na usalama nchini.
Previous Post Next Post