MH.LOWASSA AHUDHURIA MAZISHI YA KADA WA CCM SINGIDA


1 f447b
 Singida
 Februari 06,2013.
WAZIRI mkuu mstaafu Edward Lowasa, jana aliungana na maelfu ya waumini wa kanisa la KKKT, Dayosisi ya kati-Singida kwenye mazishi ya kada wa CCM, mjumbe wa kwanza wa NEC na kamati kuu (TANU) mkoa wa Singida, Mchungaji Thomas Musa.
 Katika uhai wake marehemu pia aliwahi kuwa mkuu wa kanisa hilo mwanzoni mwa miaka ya 1960, wakati huo likijulikana kanisa la KKKT-Sinodi ya kati, kabla ya kupandishwa hadhi na kujulikana kanisa la KKKT Dayosisi ya kati.

Akitoa salamu kanisa KKKT Usharika Kinampanda, Lowasa ambaye pia ni mbunge wa Monduli alisema anaheshimu mchango mkubwa uliotolewa na marehemu wakati wa uhai wake kwa jamii yote, bila kujali dini, rangi wala ukabila.

Alisema, mzee Musa kwa kuonyesha alikuwa anasimamia vema maamuzi yake, marehemu aliwahi kumuonya wakati Fulani (Lowasa) alipokuwa kiongozi wa chama (hata hivyo hakufafanua alionywa juu ya nini).

Mkuu wa mkoa Singida Parseko Kone, kwa niaba ya Rais Jakaya Kikwete ambaye hakufika kutokana na majukumu ya chama chake, mkoni Kigoma, alisema marehemu alikuwa mtendaji kazi na mfuatiliaji wa maamuzi yanayokubaliwa kwenye vikao.

Naye mwenyekiti wa CCM mkoa Singida Mgana Msindai alisema kwa niaba ya chama chake, kifo hicho kimeacha pengo kutokana na umuhimu wake na nyadhifa mbalimbali za chama alizopitia katika uhai wake.

Askofu wa KKKT Dayosisi ya kaskazini, Dk. Martine Shao alisema kwa niaba ya kanisa KKKT, jamii inapaswa kuishi kwa kufuata matendo yanayowapendeza watu wote na yeyote atayefanya hivyo, kazi zake daima zitakumbukwa hata anapokuwa amefariki dunia.

Askofu Dk. Shao alisema Thomas Musa katika uhai wake alisimamia kweli na akawataka wachungaji, wainjilisti na viongozi wa taasisi mbalimbali wote dayosisi ya kati wamuenzi marehemu kwa kufuata matendo na kazi zake nzuri, alizofanya wakati akiwa hai.

Marehemu atakumbukwa kwa mengi kutokana na mchango wake kwa jamii, hasa sekta ya afya na elimu, alipoikaibidhi serikali shule ya sekondari Mwenge na Tumaini,pia chuo cha ualimu Kinampanda na hospitali ya Kiomboi, ambayo leo hii imekuwa ya wilaya Iramba.

Wengine waliohudhuria mazishi hayo ni askofu wa dayosisi ya Meru, Paul Akyoo, askofu mstaafu dayoisi ya Dodoma Piter Masika, maaskofu wastaafu dayosisi ya kati mchungaji Gidion Maghina, Eliufoo Sima na Zephania Gunda (mkuu mstaafu wa iliyokuwa Sinodi ya kati-KKKT).

Pia baadhi ya wageni wengine katika mazishi kijijini Kinampanda alikozaliwa marehemu wilaya Iramba ni majaji kufuatia motto wa marehemu (Kipenka Musa), kuwa jaji wa mahakama ya rufaa, mbunge viti maamlum Singida Diana Chilolo na wakuu wa wilaya Iramba, Igunga na wachungaji.

Kwa mujibu wa askofu msaidizi KKKT-Dayosisi ya kati, Sprian Hilinti, Marehemu aliyezaliwa desemba 6,1927, alifariki ijumaa iliyopita, katika hospitali ya mkoa Singida kutokana na maradhi ya athma.

“Ni kweli kazi uliyoifanya ni kubwa sana katika kuliendeleza kanisa letu la KKK, Dayosisi ya kati…pumzika  mahali pema na baba zako, lala mahali pema peponi, Joshua wetu,”alisema kwa majonzi makubwa msaidizi wa askofu, mchungaji Hilinti.
MWISHO.
2 273f6
4 6ec30
Previous Post Next Post