
Majaji wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ya ICC leo wataamua iwapo kuna ushahidi wa kutosha kumfungulia mashtaka Rais wa zamani wa Ivory Coast Bw. Laurent Gbagbo ya kuhusika na ghasia ya baada ya uchaguzi nchini mwake, miaka miwili iliyopita.
Jaji kiongozi katika kesi hiyo Silvia Fernandez de Gurmendi anatarajiwa kuanza kusikiliza ushahidi huo baadaye leo ambapo waendesha mashtaka watatoa hoja zao.
Gbagbo mwenye umri wa miaka 67, ambaye ni kiongozi wa kwanza wa zamani wa taifa hilo kufikishwa kwenye mahakama ya ICC, anakabiliwa na mashtaka manne ya uhalifu dhidi ya ubinadamu, ikiwemo mauaji na ubakaji.
Kwa muda wa wiki moja, waendesha mashtaka watatoa hoja hizo mbele ya jopo la majaji watatu, ambao wataamua iwapo kuna ushahidi wa kutosha kuamini kuwa Gbagbo alihusika na uhalifu huo na hivyo anapaswa kufunguliwa mashtaka.