KATIBA MPYA TFF YAZUIWA KUTUMIKA



images 
Na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo
SERIKALI imeliagiza  Shirikisho la Mchezo wa Mpira wa Miguu nchini (TFF)  kufuta matumizi ya Katiba ya Shirikisho hilo  ya mwaka 2012 badala yake watumie Katiba ya mwaka 2006 kwa kuwa Katiba ya mwaka 2012 imekiuka kanuni  za Sheria ya Baraza la Michezo la Taifa ( BMT) Na.11 (1).

Agizo hilo limetolewa leo na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Mhe. Dkt. Fenella Mukangara alipokuwa akiongea na Waandishi wa Habari Jijini Dar es Salaam kuhusu mgogoro wa uchaguzi wa Viongozi wa TFF.
Dkt. Mukangara  pia ameiagiza TFF kufuata utaratibu wa kurekebisha Katiba za vyama vya michezo, kwa mujibu wa Sheria ya BMT iliyotungwa na Bunge pamoja na kanuni zake ambazo ziko wazi na rahisi kuzifuata.
Alifafanua kuwa TFF walikiuka Sheria Na. 12 ya Baraza la Michezo la Taifa na marekebisho yake Na.6 ya mwaka 1971 pamoja na kanuni za usajili Na. 442 za mwaka 1999.
“Kanuni ya BMT Na. 11(1) inaeleza wazi utaratibu wa marekebisho ya Katiba ambapo walitakiwa wajaze Fomu Na. 6,7,8 na 9 kisha baada ya siku 14 Msajili wa vyama vya michezo anatakiwa kuwajibu, kama anakubali anatumia Fomu Na. 11 na kama anakataa anatumia Fomu Na. 10 lakini TFF walikiuka yote haya.” Ameeleza Dkt. Mukangara
Aidha, Dkt Mukangara ameiagiza TFF kufanya uchaguzi wa Viongozi kwa mujibu wa Katiba ya mwaka 2006 kwa kuzingatia Sheria na Kanuni za BMT  na kama kuna umuhimu wa kurekebisha Katiba  waitishe mkutano Mkuu  kwa kufuata misingi ya Katiba yao ya mwaka 2006 na kanuni za BMT  kwa ajili ya kufanya maboresho hayo.
Akizungumzia taarifa zilizotolewa na vyombo vya habari kuwa FIFA watakuja nchini kufuatilia mgogoro wa TFF, Waziri amemwagiza  Msajili  wa Vyama vya michezo pamoja na TFF kuwataarifu FIFA kuhusu maelekezo yake ya kutumia Katiba ya mwaka 2006 na wawaeleze hali halisi  iliyojitokeza.
Amesema kuwa hakuna chama chochote cha michezo nchini kilicho juu ya BMT, hivyo vyama vyote na vilabu vyote  vya michezo  viendelee na shughuli zao za kuendeleza michezo kwa kuzingatia Sheria na Kanuni za BMT pamoja na Katiba zao.
Kumekuwepo na mgogoro katika mchakato mzima wa uchaguzi wa Viongozi wa TFF ikiwemo baadhi ya wagombea kulalamika kuenguliwa  na wadau mbalimbali kulalamika kuwa haki haikutendeka na wengine kuonyesha wazi  kutofuatwa kwa utaratibu wa kurekebisha Katiba hali iliyopelekea Wizara yenye dhamana ya michezo kwa kushirikiana na  BMT kuingilia kati hasa katika suala la ukiukwaji wa marekebisho ya Katiba.
Previous Post Next Post