OFISA Maendeleo wa Kusini mwa Afrika wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), Ashford Mamelodi amewasili leo kwa ajili ya kufuatilia shughuli za maendeleo ya mpira wa miguu.
Mamelodi, ambaye amekuwa msaada mkubwa kwa shughuli za maendeleo nchini Tanzania tangu alipoteuliwa kushika nafasi hiyo, pia amekuja kumtambulisha msaidizi wake, Patrick Onyango aliyeteuliwa kushika nafasi hiyo hivi karibuni.
Wakiwa nchini, wawili hao wanatarajiwa kupata taarifa ya maendeleo ya mradi wa kuweka nyasi bandia kwenye Uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza, baada ya FIFA kuipa Tanzania mradi wa nne (GOAL Project 4) wa kuweka miundombinu kusaidia maendeleo ya mpira wa miguu.
Mwanza ilipata mradi huo baada ya Halmashauri ya Jiji hilo kukubali masharti ya mradi huo ya kulipia nakisi ya fedha zinazolipwa na FIFA, ambazo ni sh. milioni 700. Mradi huo wa kuweka nyasi bandia Nyamagana utagharimu sh. milioni 900, hivyo nakisi y ash. milioni 200 italipiwa na Jiji la Mwanza.
Pia Mamelodi na Onyango watapata taarifa ya maendeleo ya Uwanja wa Gombani uliowekwa nyasi za bandia kwa msaada wa FIFA katika mradi wa GOAL Project 3; na pia kupata mikakati ya maendeleo ya TFF kwa mwaka 2013, ikiwa ni pamoja na kozi na semina mbalimbali zitakazofanyika nchini mwaka huu.
Mamelodi na Onyango pia watapata taarifa ya maendeleo ya uboreshaji wa mashindano ya Copa Coca-Cola baada ya FIFA kuingia rasmi kwenye mashindano hayo mwaka jana kwa kuendesha kozi kwa walimu wa timu za kombaini ya mikoa na waamuzi.
Kwa sasa mashindano hayo yanashirikisha vijana wenye umri chini ya miaka 17, lakini FIFA inataka yahusishe umri mdogo zaidi ili kuendeleza soka ya vijana na kushirikisha kikamilifu shule. Maofisa hao wataondoka nchini Jumatatu asubuhi.