
Na: Mwandishi Maalum
Tanzania imelitaka Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa kuendelea kuunga mkono mikakati na juhudi mbalimbali zinazolenga katika kurejesha amani ya kudumu katika eneo la Mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Wito huo umetolewa na Mhe. Tuvako Manongi,Balozi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa. Alikuwa akichangia majadiliano ya...
wazi kuhusu operesheni za kulinda amani, ujenzi wa amani na maendeleo. Majadaliano hayo yamefanyika siku ya jumatatu na kufunguliwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, na yaliandaliwa na Pakistani, nchi ambayo ni Rais wa Baraza hilo kwa mwezi huu wa Januari.
Katika mchango wake, Tanzania kupitia Mwakilishi wake , imeeleza bayana kuwa, hali iliyojitokeza mwezi Novemba mwaka jana huko Goma, ni kielelezo na ushuhuda wa dhahiri kwamba juhudi na mikakati mbadala ya ulinzi wa amani inahitajika katika kuwakabili wavurugaji wa amani katika eneo hilo.
“Ni muhimu sana kwa Baraza hili likaendelea kuunga mkono uwepo wa uwajibikaji mkubwa zaidi katika suala zima la operesheni ya kulinda amani katika DRC. Tulichokishuhudia Goma mwezi Novemba mwaka jana, ni kilelezo cha dhahiri cha kutakiwa kuwepo kwa vikosi vya kulinda amani vyenye dhamana kubwa na uwajibikaji zaidi katika kuwakabili na kuwadhibiti wavurugaji amani” akasema Balozi Manongi.
Balozi Tuvako Manongi amesisitiza ili amani ya kudumu iwepo nchini DRC, na hususani eneo hilo la Mashariki, panahitajika pia uwepo wa vikosi vya ulinzi wa amani vitakavyokuwa na uwezo wa kuchukua maamuzi ya haraka na wakati mwingine katika mazingira magumu kama sehemu muhimu ya kuchagiza ufanisi na mafanikio.
Akabainisha kwamba vikosi hivyo lazima viwe na uwezo wa kutegemewa na raia vinavyopaswa kuwalinda , na ikibidi kuwapiga ipasavyo wale wanaotaka kuendelea kuhatarisha maisha ya raia wasio na hatia.
Mwakilishi huo wa Tanzania, akaeleza zaidi kwamba vitendo vya kikatili ambavyo vimekuwa vikifanywa na makundi yenye silaha dhidi ya raia , ni ukumbusho mwingine wa kuhitajika kwa juhudi za pamoja za kutafuta amani ya kudumu katika eneo hilo.
Aidha Balozi Manongi amesisitiza kwamba ni jambo la muhimu sana kwa Umoja wa Mataifa na Taasisi za Kikanda kugawana majukumu linapokuja suala la ulinzi.
Amelihakishia Baraza kwamba katika suala hilo la DRC, litapata ushirikiano mkubwa kutoka Umoja wa Afrika ( AU), Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika ( SADC) na Mkutano wa Kimataifa kuhusu Eneo la Maziwa Makuu ( ICGLR).
Vilevile Balozi akabainisha wazi kwamba, kwa kushirikiana na taasisi za kikanda,Umoja wa Mataifa haupashwi kuhofia kupoteza wajibu wake wa msingi katika ulinzi wa amani bali ushirikiano huo unalenga katika kuleta tija na mafanikio.
Majadiliano hayo yalitanguliwa na wajumbe 15 wa Baraza Kuu la Usalama kupisha kwa kauli moja Azimio namba2086 ( 2013). Azimio hilo la kwanza la aina yake kupitishwa katika kipindi cha miaka kumi iliyopita linatambua na kuidhinisha kwamba suala la ulinzi wa amani linahitaji kushughulikiwa kwa njia au mifumo mbalimbali.
Aidha azimio hilo pamoja na masuala mengine, linasisitiza kwamba operesheni za kulinda amani lazima zifanyike katika namna ambayo itahusisha ulinzi wa amani, kuzuia kujirudia kwa migogoro na vita , kusaidia katika ujenzi wa amani endelevu , maendeleo endelevu, ujenzi wa demokrasia, utawala shirikishi na uundwaji taasisi zinazounda mfumo mzima wa serikali.
Tags:
Politics