Dk Shein Ashiriki Hafla ya Pongezi kwa Washiriki wa Gwaride la Miaka 49 ya Mapinduzi ya Zanzibar


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein akichukua Chakula wakati wa dhifa maalum ya Chakula alichowaandalia askari walioshiriki katika Maadhimisho ya miaka 49 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar katika Viwanja vya Makao Makuu ya Polisi Ziwani Zanzibar (kushoto) Makamo wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi.[Picha na Ramadhan Othman, Ikulu]
Na Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameungana na maofisa na askari wa vikosi vya Ulinzi na Usalama wa Serikali ya Jamhuri ya Mungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambao wameshiriki katika gwaride la kutimiza miaka 49 ya Mapinduzi ya Zanzibar katika chakula maalum cha mchana alichowaandali.
Hafla hiyo fupi imefanyika katika viwanja vya Polisi Ziwani mjini Zanzibar na kuhudhuriwa na viongozi mbali mbali wa vikosi vya Ulinzi na Usalama pamoja na viongozi wa Serikali akiwemo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd na viongozi wengine.
Akitoa salamu za shukurani na pongezi kwa Rais Dk. Shein kwa maandaalizi hayo maalum ya chakula cha mchana kwa vikosi hivyo, kwa niaba ya vikosi hivyo Kamanda wa Brigedia ya Nyuki Zanzibar, Brigedia Jenerali Sharif Sheikh Othman alisema kuwa hatua hiyo imewapa faraja kubwa kutokana na ushiriki wake binafsi katika chakula hicho cha mchana alichowaandalia.
Alisema kuwa hatua hiyo itavisaidia kwa kiasi kikubwa vikosi hivyo kukaa pamoja na kubadilishana mawazo ikiwa ni pamoja na kufanya tathmini ya gwaride hilo waliloshiriki hivi karibuni pamoja na kuweka mikakati ya maandalizi ya gwaride lijalo la kutimiza miaka 50 ya Mapinduzi matukufu ya Zanzibar.
Brigedia Jenerali huyo alimuhakikishia Dk. Shein kuwa vikosi vya Ulizni na Usalama vitaendelea kuimarisha ulinzi na usalama wa wananchi pamoja na mali zao.
Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Mwinyihaji Makame Mwadini akitoa neon a shukurani kutokana na ushiriki wa vikosi hivyo katika hafla hiyo, kwa niaba ya Rais wa Zanzibar, alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itaendelea kuimarisha ushirikiano na vikosi hivyo ili kuleta mafanikio zaidi.
Alisema kuwa Serikali inatambua na inathamini mchango mkubwa unaotolewa na vikosi hivyo katika masuala mbali mbali ikiwa ni pamoja na kushiriki kikamilifu katika kusimamia ulinzi na usalama wa nchi na wananchi wake, kushiriki katika maafa, michezo pamoja na ushiriki wao mkubwa katika gwaride la sherehe za Mapinduzi.
Dk. Makame alisema kuwa sherehe za kutimiza miaka 49 ya Mapinduzi matukufu ya Januari 12,1964 zilifana na kupata sifa kubwa sana kwa kila aliyeziona jambo ambalo limechangiwa zaidi na gwaride lililochezwa na vikosi hivyo ambalo lilifana sana.
Pamoja na hayo, Dk. Makame alivieleza vikosi hivyo kuwa juhudi za makusudi zitachukuliwa katika kuhakikisha changamoto zilizopo zinafanyiwa kazi kwa lengo la kujiweka tayari na kujitarisha kwa sherehe za kutimiza miaka 50 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar hapo mwakani.
Hafla hiyo ni muendelezo wa Dk. Shein katika kuvipongeza vikosi vya Ulinzi na Usalama vilivyoshiriki gwaride katika sherehe za Mapinduzi ambapo hapo mwaka jana pia, hafla hiyo ilifanyika katika viwanja vya Kambi ya Jeshi la Ulinzi na Usalama Bavuai Migombani, mjini Zanzibar kwa kuwaandalia chakula maalum cha mchana na kula nao pamoja.
Sambamba na hayo, Dk. Shein aliwaandalia chakula cha mchana vijana wa Chipukizi na Halaiki walioshiriki katika maadhimisho ya miaka 48 ya Mapinduzi huko katika hoteli ya Bwawani mjini Zanzibar ambapo pia, Dk. Shein amewaandalia chakula hicho maalum cha vijana hao katika hoteli hiyo hapo kesho.
Previous Post Next Post