BINGWA wa ngumi wa uzito wa kati Tanzania, Francis Cheka amesema amejiandaa kucheza raundi zote 12 kwenye pambano lake la kuwania ubingwa wa IBF Afrika dhidi ya Chiotra Chimwemwe wa Malawi.
Mabondia hao kesho watapima uzito na afya kwenye Ukumbi wa Tripple A, kabla ya pambano lao siku inayofuata kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.
“Mashabiki wangu wamezoea kuona nashinda raundi ya sita au ya saba, lakini kwa Mmalawi nimejiandaa kucheza raundi zote 12,” alisema bondia huyo anayenolewa na kocha Abdallah Salehe.
Tayari mabondia wote wamekwishawasili Arusha tangu wiki iliyopita licha ya kila mmoja kukwepa kuonana na mwenzake na kesho watakutana kwa mara ya kwanza wakati wa kupima uzito.
“Nimesikia Chimwemwe yuko hapa tangu Alhamisi na kocha wake, Daudi Kikwanje, niliomba kuonana naye amegoma huenda ana imani zake,” alieleza Cheka kwa njia ya simu kutoka Arusha.
Akizungumzia maandalizi yake kabla ya kupanda ulingoni, Cheka alisema kocha wake amefanya kazi ya ziada kuhakikisha anatwaa mkanda huo na kusisitiza hategemei kumwangusha kwenye pambano hilo.
“Natambua ugumu wa mpinzani wangu na mara nyingi wachezaji kutoka nje wanaposikia wanacheza na Cheka wanajiandaa kikamilifu lakini hilo mimi halinisumbui hata kidogo,” alitamba bondia huyo.