LAGOS, NIGERIA MWIGIZAJI nyota wa Nollywood, Kenneth Okonkwo 'Andy' ameitaka Serikali ya Nigeria kuchukua jukumu la kumtibu msanii Ngozi Nwosu. Ngozi amekuwa akikabiliwa na matatizo ya ini hali inayomfanya ashindwe kutekeleza kazi zake za uigizaji kwa miezi kadhaa sasa. Okonkwo alisema kitendo cha Serikali kukaa kimya bila msaada kwa msanii huyo, kinaleta picha mbaya kutokana na ukweli kwamba wasanii wamekuwa sehemu ya taswira ya taifa kimataifa. Alisema hali ya msanii mwenzake si nzuri na kwamba anapaswa kupata matibabu nje ya nchi na si kumwacha akiteseka Nigeria. "Ngozi kwa kiasi kikubwa amechangia maendeleo ya tasnia ya sanaa nchini. Huu ni muda kwa Serikali kumshika mkono ili kunusuru maisha yake," alisema Andy. "Ameigiza sinema nyingi zilizoitangaza Nigeria nje ya nchi. Nichukue nafasi hii kumshukuru Gavana Babatunde Fashola wa Lagos aliyejitokeza kuchangia matibabu ya Ngozi. Nawasihi viongozi wengine wajitokeze kuokoa maisha yake. "Matatizo aliyonayo ni makubwa. Sisi waigizaji wa Nollywood tuna nafasi yetu. Tumeshaanza kuchanga fedha ili mwenzetu apate matibabu." |
Tags:
Entertainment
