Mbunge wa Ubungo kwa tiketi ya Chadema, John Mnyika akiwa na aliyekuwa mgombea wa ubunge kwa tiketi ya CCM katika uchaguzi Mkuu 2010,Hawa Ng’umbi, mwezi Mei 2012 siku Mnyika alipo shinda kesi.
Na Mo blog
Wapinzani wa kisiasa, mbunge wa Ubungo John Mnyika (CHADEMA), na aliyekuwa mpinzani wake kwenye kinyang’anyiro cha kuwania wadhifa huo katika Uchaguzi Mkuu wa 2010, Hawa Ng’umbi (CCM), kwa mara nyingine tena leo wanatarajiwa kupambana kwa hoja za kisheria wakati wa usikilizwaji wa rufaa ya Ng’umbi ya kupinga hukumu ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, iliyomthibitisha Mnyika kuwa mbunge halali wa Ubungo.
Katika hukumu hiyo iliyotolewa Mei 24, 2012, Jaji Upendo Msuya alisema upande wa madai ulishindwa kuyathibitisha madai yake pasi na shaka, huku akidai kuwa ushahidi wa Ng’humbi ulikuwa ni maneno ya kusikia tu ambayo hakuyashuhudia.
Hata hivyo, Ng’umbi hakukubaliana na hukumu hiyo na kuamua kukata rufaa akiiomba mahakama ya rufani itengue hukumu hiyo ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam. Rufaa hiyo imepangwa kuanza kusikilizwa leo na Jopo la Majaji watatu wa Mahakama ya Rufani; Salum Massati, Katherine Oriyo na Nathalia Kimaro.
Baadhi ya hoja zake katika rufaa hiyo, Ng’umbi anadai kuwa jaji alikosea kusema kuwa makosa yaliyobainika katika ujumlishaji na kuhesabu kura na kusababisha kuwapo kwa kura 14,854, zisizohesabiwa hayakuathiri matokeo ya uchaguzi.
Anadai kuwa alithibitsha makosa katika mchakato wa uchaguzi yaliyosababisha kuwapo kwa kura 14, 854 zisizohesabiwa, hivyo jaji alikose kwa kutokuhamishia kwa mdaiwa, jukumu la kuelezea sababu za kuwapo kwa dosari hizo.
Tags:
Social
