Takriban watu 6 akiwemo mtoto mmoja wameripotiwa kufa Wilayani Pangani mkoani Tanga kwa kula Samaki aina ya Kasa.
Wakazi wanaoishi katika vijiji vilivyopo pembeni mwa bahari ya Hindi nchini, wameonywa kuacha kitendo cha kuwinda na kuua viumbe wa bahari wanaohifadhiwa kisheria aina ya ''kasa'' kwa sababu baadhi yao wana sumu ambayo imesababisha watu sita kufariki dunia akiwemo mtoto wa miezi sita kwa sababu ya kula nyama yake.
Afisa mradi wa shirika la hifadhi ya viumbe vyenye hatari ya kutoweka baharini Bwana Boniveture Mchomvu amewaambia viongozi wa serikali ngazi ya wilaya ya Pangani kuwa baadhi ya wavuvi wamekuwa wakiwawinda kasa katika fukwe za bahari ya hindi ambao wamekuwa wakitaga mayai kisha kurudi baharini hatua ambayo imesababisha kasa kuwa katika hatari ya kutoweka.
Kwa upande wake mhifadhi wa hifadhi inayohifadhiwa kisheria na serikali ya samaki aliyepotea miaka 200 iliyopita aina ya Silikanti Bi. Anita Jullius amesema uvuvi haramu unaofanywa na baadhi ya wavuvi wa ndani na nje ya nchi wa kutumia baruti na nyavu ndogo katika hifadhi za bahari ya Hindi umesababisha miamba bahari inayohifadhi Kasa kuvunjwa, hatua ambayo imesababisha viumbe hao kupungua na kuikosesha mapato serikali.
Kufuatia hatua hiyo Afisa Uvuvi wilayani Pangani Bwana Chitambo Kauta amesema wavuvi haramu wa kutumia baruti wanatokea katika wilaya za Bagamoyo, Tanga na eneo la Kigombe ambapo wanapofanya milipuko huharibu matumbawe ambayo ndio mazalia ya samaki hivyo wanafanya doria lakini tatizo linalowakabili ni raslimali fedha.