WAZIRI WA FEDHA, DR. WILLLIAM MGIMWA AFARIKI DUNIA BAADA YA KUUGUA MUDA MREFU!

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amepokea kwa mshtuko na huzuni kubwa taarifa za kifo cha Waziri wa Fedha, Mheshimiwa William Mgimwa, aliyekuwa pia Mbunge wa Jimbo la Kalenga (Mkoa wa Iringa) kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM).

Rais Kikwete amesema kuwa taifa limempoteza Waziri Mgimwa katika kipindi lilipokuwa linamhitaji zaidi kutokana na mchango wake mkubwa ambao amekuwa akiutoa kupitia nafasi zake za Waziri wa Serikali na mwakilishi wa wananchi wa Jimbo la Kalenga.

Kifo cha Mheshimiwa Mgimwa kimetangazwa mchana wa leo, Jumatano, Januari Mosi, 2014, na Katibu Mkuu Kiongozi (KMK) Balozi Ombeni Sefue kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katika tangazo lake, Balozi Sefue amesema kuwa Waziri Mgimwa ameaga dunia asubuhi ya leo saa 5:20 (Saa za Afrika ya Kati) katika Hospitali ya Kloof Medi-Clinic , Pretoria, Afrika Kusini ambako amekuwa amelazwa kwa muda sasa.

Balozi Sefue amesema kuwa maandalizi ya kuurudisha nyumbani mwili wa Waziri Mgimwa yanafanywa na Serikali kwa kushirikiana na familia yake na kuwa taarifa zaidi za suala hilo zitatolewa baadaye kwa kadri zinavyopatikana na maandalizi yanavyoendelea.

Katika salamu zake kwa Waziri Mkuu Mheshimiwa Mizengo Pinda na kwa familia ya Marehemu Mgimwa, Rais Kikwete amesema: “Sina maneno ya kutosha kuelezea mshtuko na huzuni yangu kubwa kufuatia taarifa za kifo cha Mheshimiwa Mgimwa.

Binafsi nimemtembelea mara mbili kwenye Hospitali alikokuwa amelazwa na mara ya mwisho hali yake ilikuwa imeimarika. Tulizungumza kwa kiasi cha dakika 10 hivi akanielezea nia yake na tamaa yake ya kurejea nyumbani kwa sababu hali yake ilikuwa nzuri.”

Ameongeza Mheshimiwa Rais Kikwete: “Sote tunajua mchango wake katika Serikali. Sote tulitamani kuendelea kuwa naye, lakini haya ni mapenzi ya Mungu.”

“Napenda kutoa pole nyingi na rambirambi zangu za dhati kwa wana-familia wote kwa kuondokewa na mhimili wao. Naungana nanyi katika kuomboleza msiba huo mkubwa. Napenda mjue kuwa msiba huu ni msiba wangu pia. Machungu yenu ni majonzi yangu,” amesema Rais Kikwete.

Rais pia amewatumia rambirambi wananchi wa Jimbo la Kalenga akisema kuwa wamempoteza mwakilishi na mtetezi mahiri wa maslahi yao.

Mgimwa aliyezaliwa January 20, 1950 na kuwa mbunge wa jimbo la Kalenga mkoani Iringa kupitia chama cha Mapinduzi (CCM)

Dk. Mgimwa alikuwa mkufunzi katika Chuo cha Benki mkoani Mwanza, kabla ya kufanikiwa kuchaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo la Kalenga, Mkoa wa Iringa, katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.

Historia fupi ya Waziri wa Fedha wa Tanzania, Dr. William Mgimwa aliyefariki dunia nchini Afrika Kusini alipokuwa amelazwa kwa matibabu.

Kuzaliwa: Januari 20, 1950 Kalenga Iringa.

Elimu:

1966 - 1967 Shule ya Msingi Tosa
1961 -1965 Shule ya Msingi Wasa
1970-1971 Seminari ya Mafinga
1968 - 1969 Tosamaganga Sekondari
1975 - 1984 Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) - Postgraduate in Finance
1989 - 1991 IDM Mzumbe (MBA - Finance)

Ajira

1981 - 2000 - NBC Ltd (Mhasibu, Mhadhiri, Mkurugenzi, Mkurugenzi Mkuu)

2000 - 2010 - Chuo cha Benki Kuu ya Tanzania Mwanza (Mkuu wa Chuo)

2010 - 2013 - Mbunge, Kalenga (CCM)

Kufariki: Januari 1, 2014

Bongo61 Inatoa Pole kwa Wanafamilia na Taifa Kwa Ujumla, Kwani Bwana Alitoa na Bwana  Ametwaa Jina lake Liinuliwe.

Previous Post Next Post

Popular Items

WAKUU WA USALAMA KUHOJIWA KENYA