NCHI NYINGI ZAUNGA MKONO MAKUBALIANO KUHUSU SILAHA ZA SYRIA:


zzzzzzzzzzmakubaliano_d80de.jpg
Makubaliano yaliyofikiwa kati ya Marekani na Urusi kuhusu kuteketezwa silaha za kemikali za Syria, yameungwa mkono na nchi nyingi muhimu duniani. Ujerumani, China, Ufaransa na Israel ni miongoni mwa nchi hizo.
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani ameyataja makubaliano hayo kuwa ni "yenye kutoa dalili njema ya matumaini."
Wizara ya mambo ya nchi za nje ya China imesema kuwa makubaliano hayo yatasaidia kupunguza mvutano ndani ya Syria. Waziri wa mambo ya nchi za nje wa China Wang Yi ameyasema hayo baada ya mazungumzo na mwenzake wa Ufaransa Laurent Fabius mjini Beijing.
Israel pia imeyakaribisha makubaliano hayo, japo kwa tahadhari. Yuval Steinitz, waziri wa masuala ya kimkakati wa nchi hiyo ambaye ni mshirika wa karibu wa waziri mkuu Benjamin Netanyahu amesema kama ilivyo kwa makubaliano yote mengine, umuhimu wa haya utategemea namna yatakavyotekelezwa.
Matokeo ndio kipimo
Steinitz amesema makubaliano haya juu ya kuteketezwa kwa silaha za kemikali za Syria yana faida na hasara zake. ''Faida ni kwamba yanahusisha uwajibikaji wa Syria yenyewe kushiriki katika kuangamiza silaha hizo, na kutoa ahadi ya kutozitengeneza tena'', amesema waziri huyo na kuongeza kuwa hasara ni kwamba mpango huu unatoa muda mrefu wa kutekelezwa kwa zoezi la kuharibu silaha hizo.
Hata hivyo, waasi wanaopigana dhidi ya serikali ya rais Bashar al-Assad wameyakosoa vikali makubaliano hayo. ''Hatuwezi kukubali sehemu yoyote ya mpango huo'' amesema kamanda wa jeshi la waasi hao, Jenerali Selim Idris. ''Je sisi raia wa Syria, tutalazimika kusubiri hadi mwaka 2014, tukiuawa kila siku, kwa sababu tu makubaliano hayo yanataka silaha za sumu ziwe zimeangamizwa mwaka 2014?'', ameshangaa kamanda huyo.
Bado upo uwezekano wa mashambulizi
Akitangaza makubaliano baina yake na waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov, waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry ameitaka Syria kufungua milango ili wakaguzi wa shirika la kimataifa la kudhibiti silaha za kemikali, OPCW, waweze kufanya kazi bila kipingamizi. Kerry alisema ifikapo mwezi Novemba, wakaguzi hao watakuwa tayari wamewasili Syria.
Ingawa Lavrov amepinga vikali matumizi yoyote ya nguvu dhidi ya mshirika wake Syria, Kerry amesema hakuna maafikiano yoyote yanayoweza kufikiwa, kuhusu hatua zitakazochukuliwa ikiwa Syria itaonyesha ukaidi.
Rais Barrack Obama wa Marekani amesema kwa sasa mpira ametupiwa rais Bashar al-Assad, na kuonya kuwa bado upo uwezekano wa Marekani kuishambulia kijeshi Syria ikiwa itashindwa kutimiza matakwa ya makubaliano ya kuangamiza silaha zake za kemikali.
Previous Post Next Post