BAKHRESA ANUNUA BANDARI SC YA LIGI KUU ZANZIBAR


azam 3fc17
Alhaj Said Salim Awadh Bakhresa, baada ya Azam FC sasa aja na timu ya Bandari SC ya Ligi Kuu Zanzibar (HM)

SIKU chache baada ya Shirika la Bandari Zanzibar kujivua jukumu la kuiendesha timu yake ya soka Bandari SC, uongozi wa timu hiyo umeamua kuiuza nafasi yake kwa makampuni ya S.S. Bakhresa yanayomiliki klabu ya Azam FC ya Dar es Salaam.

Uamuzi wa kuuza daraja hilo la ligi kuu kwa matajiri hao wa ngano, ‘ice cream’ na boti za Azam Marine, umefikiwa katika mkutano wa wanachama na uongozi wa timu na shirika, uliofanyika Julai 1, mwaka huu.
 
Aidha, orodha yenye majina ya wanachama hao, imeambatanishwa na barua hiyo kwenda ZFA Taifa.
 
Katibu Mkuu wa Azam FC, Nassor Idrissa Mohammed ‘Father’, alikiri kuwa uongozi wa timu yake umeshakaa mezani na wenzao wa Bandari, na tayari wamekubaliana kwa mauziano hayo.
 
Hata hivyo, alisema kwa sasa wamewapa kazi wanasheria wao, kuangalia sheria na kanuni za ZFA zinaelekeza nini kabla kumalizana na Bandari.
 
Kuhusu tetesi kwamba awali walitaka kununua daraja la klabu ya Malindi iliyoteremka daraja kutoka ligi kuu hadi la kwanza taifa, Idrissa alisema hawana mpango huo kwani lengo lao ni kucheza ligi kuu moja kwa moja.
 
Naye Katibu wa Bandari SC Makame Silima Makame, akizungumza hatima ya wachezaji wa kikosi cha timu yake baada ya kuuza daraja lao, alisema wanakusudia kununua nafasi katika ligi ya daraja la pili msimu ujao, ili waendelee kuwemo kwenye soka.
 
Hata hivyo, alisema hatua hiyo itafanyika baada ya kumaliza mchakat wa kuuza daraja lao kwa Azam FC. Chanzo: Salum Vuai, Zanzibar
Previous Post Next Post