WASHAMBULIAJI WA TAIFA STARS SAMATA NA ULIMWENGU KUTUA NCHINI






TanzaniaFootballFederation1 c41eb


Release No. 020
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Februari 2, 2013
SAMATA, ULIMWENGU MBIONI KUTUA NCHINI
Washambuliaji wa Taifa Stars, Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu wanatarajia kutua nchini kesho (Februari 3 mwaka huu) tayari kwa mechi ya Cameroon itakayochezwa Jumatano kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Samata na Ulimwengu wanaochezea timu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) watawasili saa 11.10 jioni kwa ndege ya PrecisionAir na kwenda moja kwa moja kambi hoteli ya Tansoma.
Wachezaji wa Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager wanaanza kuripoti kambini leo jioni (Februari 2 mwaka huu) mara baada ya mechi kati ya Yanga na Mtibwa Sugar.
Mechi hiyo iliyo katika Kalenda ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) pia itatumika kwa ajili ya kutoa ujumbe wa vita dhidi ya Malaria viwanjani, ugonjwa unaoongoza barani Afrika kwa kusababisha vifo vya watoto na wajawazito.
TFF kama ilivyo Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) na FIFA imekuwa msitari wa mbele katika kueneza kampeni ya vita dhidi ya Malaria inayoongozwa United Against Malaria (UAM). Rais wa TFF, Leodegar Tenga na nahodha wa Cameroon, Samuel Eto’o ni miongoni mwa mabalozi wa vita dhidi ya Malaria barani Afrika.
WACAMEROON KUANZA KUTUA DAR KESHO
Kundi la kwanza la Cameroon likiongozwa na kiungo wa zamani wa Toulouse ya Ufaransa ambaye sasa yuko Al Ahli ya Falme za Kiarabu (UAE), Achille Emana na Meneja wa timu hiyo Rigobert Song litatua nchini kesho (Februari 3 mwaka huu) saa 4.40 usiku kwa ndege ya KLM.
Wachezaji wengine katika kundi hilo ni Vincent Aboubakary anayechezea timu ya Valenciennes iliyoko Ligi Kuu ya Ufaransa, kipa Charles Itandje anayedakia timu ya POAK FC ya Ugiriki, Kocha wa viungo Sylvain Monkam.
Mshambuliaji wa Anzhi Makhachkala ya Urusi ambaye ndiye nahodha wa Cameroon, Samuel Eto’o ataongoza kundi la pili litakalowasili nchini Februari 4 mwaka huu (saa 3.45 asubuhi) kwa ndege ya Kenya Airways kupitia Nairobi, Kenya.
Wengine katika ndege hiyo Herve Tchami wa Budapest Honved ya Hungary, beki Nicolas Nkoulou wa Marseille ya Ufaransa, mshambualiji Jean Paul Yontcha wa SC Olhanense ya Ureno na daktari wa timu Dk. Boubakary Sidik wakati Kocha wa timu hiyo Jean Paul Akono na msaidizi wake Martin Ndtoungou watawasili saa 4.40 asubuhi kwa ndege ya Kenya Airways akitokea Afrika Kusini.
Februari 4 mwaka huu kuna kundi lingine litakaloingia saa 4.40 usiku kwa ndege ya KLM ambalo lina beki Jean Kana Biyick wa Rennes ya Ufaransa, mshambuliaji Fabrice Olinga wa Malaga FC ya Hispania, beki Allan Nyom wa Udinese ya Italia ambaye yuko kwa mkopo Granada ya Hispania na beki wa kushoto Henri Bedimo wa Montpellier ya Ufaransa.
Wachezaji waliobaki wakiongozwa na kiungo wa Barcelona, Alexandre Song watawasili Februari 5 mwaka huu kwa muda tofauti kwa ndege za KLM na Kenya Airways.
TENGA AONGEZA WAWILI KAMATI YA NIDHAMU
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga ameteua wajumbe wawili kuingia kwenye Kamati ya Nidhamu ya TFF baada ya nafasi mbili kuwa wazi kutokana na mmoja kuteuliwa kuongoza kamati nyingine ya TFF na mwingine kufariki dunia.
Iddi Mtiginjolla ambaye alikuwa mjumbe wa Kamati ya Nidhamu hivi karibuni aliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF baada ya Shirikisho kufanya mabadiliko ya katiba yaliyotokana na maagizo ya Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Mpira wa Miguu (FIFA), wakati mjumbe mwingine wa Kamati ya Nidhamu, Shaaban Semlangwa alifariki dunia katikati ya mwaka uliopita.
Wajumbe wapya walioteuliwa ni Jesse Mguto- alikuwa Hakimu Mkazi na kwa sasa ni mwanasheria na Wakili wa Mahakama Kuu. Ana Digrii ya Sheria. Mwingine ni Yohane Masala ambaye kwa sasa ni Mwanasheria Mwandamizi wa Serikali (Principal State Attorney). Ana Digrii ya Kwanza na ya Pili ya Sheria na Digrii ya Pili katika masuala ya Amani na Haki (MA in Peace and Justice).
Rais Tenga amesema ana imani na uwezo wa watu hao na kwamba watafanya kazi yao kwa uadilifu ili Shirikisho liendelee kuboresha utawala bora.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
Previous Post Next Post