TASAF YATUA UMOJA WA MATAIFA


UN1 11f3f
 Na Mwandishi Maalum
  Mfuko wa Maendeleo ya  Jamii (TASAF) umeelezwa kama mfano halisi unaoweza kuigwa  na jumuiya ya kimataifa hususani katika eneo la   uwezeshaji  wa kipato kwa  wananchi maskini,dhana ya ushirikishwaji, upunguzaji wa umaskini , upatikanaji wa ajira na ulinzi wa Jamii.

“ tunaweza  kujifunza mengi kutoka TASAF ni mfuko ambao unafanya kazi kubwa na nzuri, nimekwenda Tanzania nimejionea mwenye. Wakati mwingine ili kufahamu  lipi linawezekana, na lipi haliwezekani, ni jambo jema sana kama ukienda na kushuhudia mwenyewe badala ya kusoma au kusikia kutoka  kwa watu wengine”
Hiyo ilikuwa ni kauli ya  Bw. Mawutor Ablo, Mkurugenzi wa  Ulinzi wa Jamii, Wizara ya Ajira na Ustawi wa jamii nchini Ghana. Bw. Ablo alikuwa mmoja wa wana-jopo watano waliokuwa wakichangia  majadiliano ya mada iliyohusu “ Mwelekeo wa Jamii katika Ajenda ya Kimataifa ya  Maendeleo baada ya  mwaka 2015.
Majadiliano hayo ni sehemu ya   mada kadhaa zinazohusu  Mkutano wa 51 wa Kimisheni ya Maendeleo ya Jamii, mkutano huu wa wiki moja  ambao maudhui yake ni “ kukuza uwezeshaji wa watu katika kufanikisha uondoaji wa umaskini, ushirikiano wa kijamii, ajira kamili na zenye tija”,  unafanyika hapa  Makao  Makuu ya Umoja wa  Mataifa ukiwashirikisha mawaziri, wanazuoni, watafiti wa masuala ya kijamii  na taasisi zisizo za kiserikali.
Bw. Mawutor Ablo amekwenda mbali zaidi kwa kusema tunapojadiliana kuhusu kile tunachotakiwa kufanya baada ya 2015, miradi kama ya TASAF inatakiwa kuchukuliwa kama sehemu ya mafaniko na mfano wa kuigwa. Wala hatuna sababu ya kwenda mbali, mifano hai na yenye mafanikio ipo”. akasisitiza.
Kauli hiyo ya Bwa. Ablo iliungwa mkono na mwana-jopo mwingine, Dkt. Timo Voipio ambaye ni Mshauri  Mwandamizi  kuhusu Sera ya Jamii  na Kazi za  Heshima katika  Wizara ya Mambo ya Nje ya  Norway.
Yeye alieleza kwamba licha ya kwamba tafiti zake nyingi kuhusu maendeleo ya jamii amezifanyia Afrika, lakini pia  ameishi Tanzania kwa miaka kadhaa na  amejionea mwenyewe kazi nzuri inayofanywa na TASAF
“ inawezekana kabisa kuwa na sera za ulinzi wa jamii, uwezeshaji wao,  kuwapunguzia makali ya umaskini na kubwa zaidi ushirikishwaji katika maamuzi ya mambo yanayowahusu”. Nimeyaona haya kupitia TASAF, inawezekana kukawa na ugumu katika kubadili  mfumo wa maisha  hususani kwa  mwananchi maskini ambaye amezoea  kulima muhogo ukamwambia alime mahindiaina” akasema Dkt. Voipio.
Lakini  hili inawezekana kwa kupitia miradi kama ya  TASAF ambayo inasisitiza sana ushirishwaji wa wananchi wenyewe” kwa mujibu wa  Dkt. Timo Voipio
Akizungumzia kuhusu viashiria vya maendeleo ya binadamu, bila ya kuingia kwa udani,  Dkt. Voipio anasema Tanzania na Kenya kama nchi jirani zina ushindani Fulani linapokuja suala la viashiria zima la viashiria hivyo kila nchi ikijitahidi kuipiku nyingine. Ushidani ambazo anasema anaamini unafanyika katika nchi nyingi majirani.
Naye mshiriki mwingine wa majadiliano hayo,  Bwa, Stephen Pursey, ambaye ni Mkurugenzi wa Muunganiko wa Sera na mshauri wa  Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la kazi duniani ( ILO) yeye alibainisha kwamba suala la  upatikanaji wa ajira ni jambo ambalo limekuwa likizungumzwa na kujadiliwa na kila mtu achia mbali serikali.
Hata hivyo anasema ingawa  ukosefu wa ajira  ni tatizo linaloendelea duniani kote. Bado anaamini kuwa ajira zinaweza kutengenezwa  kupitia ubunifu wa sera na kuwajibika.
Akasema bado anakumbuka kauli ya Bado  Rais Mstaafu wa Tanzania Benjamin Mkapa ambaye katika mikutano  ya  Kamisheni
kuhusu Athari za Utadawazi katika Jamii,alivyokuwa  akielezea namna alivyokuwa akiwabana mawaziri wake wanapowasilisha maandiko yao katika Baraza la  Mawaziri
“ Mkapa alikuwa akitueleza kwamba kila waziri aliyekuwa anawasilisha  mpango wake katika Baraza la Mawaziri alikuwa akimuuliza ni ajira ngapi zitazalishwa kutoka na mpango au mradi unaowasilishwa”.
Ni  wazi kwamba ufuatiliaji wa aina hii uliwafanya mawaziri husika kuhakikisha kwamba suala la ajira lilikuwa linapewa uzito wa peke yake, na hili ni jambo ambalo linaweza kuwa mfano wa kuigwa   kama kweli tunataka kupunguza tatizo la ajira hususani kwa vijana” akasisitiza Bw. Stephen Pursey
Akasema ajira  au uwezeshaji wa kipato si lazima ziwe kazi za maofisini tu. Hata kwa kuwapatia wanakijiji tenda ya kutengeneza madawati  kwaajili ya shule yao, au ujenzi wa barabra ya  eneo lao, tayari unakuwa umewapatia ajira na kipato hataka kama ajira hiyo ni ya muda lakini tayari  umewawezesha.
Kama hilo halitoshi, Mtaalamu huyo kutoka ILO alikwenda mbali zaidi kwa   kusisitiza haja na umuhimu wa kuwa na vipaumbele vinavyotekelezeka.
Anasema  haiwezekani  kuwa na vipaumbele vingi, tafsri ya kuwa na vipaumbele vingi  iwe katika eneo lolote lile, maana yake ni moja tu huna kipaumbele.
Akaongeza kwamba watu wanajua  nini wanataka hata kama watu hao ni maskini, wanajua nini wanataka wakati gani, mahali gani na kwa mazingira gani, kwa  hiyo tunapotafakari  nini kifanyike  baada ya 2015 lazima pia tuheshimu matakwa ya watu, wao wanajua nini wanataka badala ya kuwapandikizia au kuwaamulia.
Muhimili wa Maendeleo ya Jamii, ni kati ya mihimili mitatu inayounda maendeleo endelevu na  ambayo Jumuiya ya Kimataifa imekuwa  ikiyafanyia kazi  katika nyanja mbalimbali  hususani kupitia utekelezaji wa   Malengo ya Maendeleo ya Millenia na mkazo mkubwa  ukiwa katika kupunguza au kuondoa umaskini,  kupungua pengo  kati ya walio nacho na wasio nacho, utafutaji wa vyanzo  vya ajira hususani kwa vijana, ulinzi wa jamii, elimu, hifadhi ya mazingira na ukuaji wa uchumi.
Kupitia mkutano huu wa Kamisheni ya  Maendeleo ya Jamii washiriki  wanajadiliana na kukusanya mawazo ambayo yatachangia katika maadalizi ya sera ya Jamii na kuchangia mwelekeo vipaumbele vya nini kifanyike baada ya mwaka 2015, mwaka ambao  utekelezaji wa  Malengo  Nane ya  Maendeleo ya Millenia  utafikia   ukingoni.
Previous Post Next Post