“MAJI; KWA NGUVU YA UMMA”:WARAKA WA MNYIKA (MB) KWA WANANCHI


2-wakipinga  3a972
Waraka wa Kwanza kwa mwaka 2013 wa Mbunge kwa Wananchi
“Maji; kwa Nguvu ya Umma”:
Waheshimiwa Wananchi wenzangu, Katiba ya Nchi pamoja na ubovu wake
inatamka katika Ibara ya 63 (2) kwamba “Sehemu ya pili ya Bunge itakuwa ndicho
chombo kikuu cha Jamhuri ya Muungano ambacho kitakuwa na madaraka, kwa
niaba ya wananchi kuisimamia na kuishauri Serikali ya Jamhuri ya Muungano
na vyombo vyake vyote katika utekelezaji wa majukumu yake kwa mujibu wa
katiba”.

Hata hivyo kutokana na uzembe wa uongozi wa Bunge wa kushindwa kuzingatia
na upuuzi wa wabunge wengi wa CCM kuridhia hoja ya kuondolewa hoja yangu
binafsi; Bunge limeshindwa kutimiza wajibu wake wa kuisimamia Serikali kuhusu
hatua za haraka za kuboresha upatikanaji wa maji safi na ushughulikiaji wa maji
taka katika Jiji la Dar es Salaam.

Katiba ya Nchi ibara ya 8 (1) inatamka kwamba Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ni nchi inayofuata misingi ya demokrasia na haki ya kijamii kwa hiyo
wananchi ndio msingi wa mamlaka yote, na serikali itapata madaraka na mamlaka
yake yote kutoka kwa wananchi kwa mujibu wa katiba.

Ibara hiyo inaendelea kueleza kwamba lengo kuu la serikali ni ustawi wa
wananchi, Serikali itawajibika kwa wananchi na wananchi watashiriki katika
shughuli za Serikali yao kwa mujibu wa masharti ya katiba hii.

Kwa kuwa wananchi mmekoseshwa fursa ya kushiriki kupitia mwakilishi wenu
niliyewasilisha hoja binafsi kwa kuzingatia wajibu wa kibunge na mamlaka ya
madaraka ya Bunge kwa mujibu wa ibara ya 63 na 100 ya Katiba ya Nchi; kwa
waraka huu naiwasilisha hoja binafsi yangu kwenu wananchi muijadili na kufanya
maamuzi mtayoona yanafaa.

Nawaomba mfanye maamuzi ya kuunganisha nguvu ya umma kuiwajibisha
Serikali iwajibike kwenu kwa kuchukua hatua tisa za haraka, kuboresha
upatikanaji wa maji safi na ushughulikiaji wa maji taka katika Jiji la Dar
es salaam na nchi nzima kama nilivyopendekeza kwenye hoja binafsi.
(NIMEAMBATANISHA NAKALA).

Hoja hii kwa kuwa wameiondoa katika bunge linaloongozwa na CCM na Serikali;
naiwasilisha kwenye ‘bunge’ la wananchi ambalo ndio msingi wa mamlaka na
madaraka yote.

Unganisheni nguvu ya umma kwa njia zozote mtazoona zinafaa kwa kurejea katiba
ya nchi hususan ibara ya 18 ya uhuru kupewa taarifa na kutoa maoni; ibara ya 20
ya uhuru kujumuika na kutoa mawazo hadharani kupitia mikutano na maandamano
na ibara ya 21 ya haki na uhuru wa kushiriki kwa ukamilifu katika kufikia uamuzi
juu ya mambo yanayokuhusu wewe, maisha yako na yanayolihusu taifa.

Ukipata waraka huu na hoja binafsi sambaza kwa mwenzako na utujulishe
maamuzi mtayofikia kupitia mbungeubungo@yahoo.com au 0768774274 au SLP
62066 Dar es Salaam ili tushirikiane kuwezesha uwajibikaji kwenye sekta ya maji
kwa nguvu ya umma.

Kilichojiri kabla na wakati wa Bunge kuhusu Hoja Binafsi ya Upatikanaji
Maji Safi na Ushughulikiaji wa Maji Taka Jijini Dar es Salaam:

Kutokana na umuhimu wa hoja ya Hatua za Haraka za Kuboresha Upatikanaji wa
Maji Safi na Ushughulikiaji wa Maji Taka kwa maisha ya wananchi wa Dar es
Salaam na Nchi kwa ujumla, tarehe 8 Januari 2013 niliwasilisha TENA taarifa ya
hoja hiyo ili kutimiza masharti ya kanuni za Bunge ambayo yanaelekeza kuwa hoja
isipowasilishwa na kujadiliwa taarifa yake inatenguka.

Nilitaka pia maelekezo ili kuwasilisha marekebisho zaidi na maelezo ya ziada kwa
kuwa katika taarifa hiyo, nilipanua kusudio na wigo wa hoja husika kuwa nchini
kwa kuzingatia yaliyojiri wakati na baada ya mkutano wa tisa wa Bunge kuhusu
masuala husika.

Tarehe 10 Januari 2013 niliruhusiwa kuwasilisha mabadiliko na maelezo ya
nyongeza na Ijumaa tarehe 1 Februari 2013, niliwasilisha mabadiliko ya hoja na
maelezo ya nyongeza kwa kuzingatia kanuni ya 55 (10) ambayo inaruhusu mbunge
kufanya mabadiliko ya hoja yake iwapo atatoa taarifa kutaka kufanya mabadiliko
walau siku moja kabla ya siku ile ambapo hoja hiyo itawekwa kwenye orodha ya
shughuli ili ijadiliwe.

Jumapili tarehe 3 Februari 2013 nilitafutwa jioni na kupewa barua iliyogongwa
muhuri wa SIRI kuwa nimekataliwa kufanya mabadiliko na maelezo yangu ya
nyongeza yamerudishwa, tafsiri yake ni kuwa nilitakiwa kuwasilisha maelezo na
hoja kama yalivyokuwa Novemba 2012 kabla ya kauli ya Serikali Bungeni ya
tarehe 7 Novemba 2012.

Vyanzo vyangu ndani ya Serikali, Bunge na CCM vilishanidokeza kuwa lengo
lilikuwa ni kuiondoa hoja hiyo kwa majibu mepesi kuwa ina tarehe zenye
kuonyesha kuwa ‘imepitwa na wakati’.

Tarehe 4 Februari 2013 asubuhi kabla ya kuingia bungeni kuwasilisha hoja hiyo
niliwasilisha majibu ya barua kwa Katibu wa Bunge ya kupinga mabadiliko na
maelezo ya nyongeza kukataliwa kwa kuzingatia kuwa sababu nilizoandikiwa
hazikuwa za msingi na barua hiyo iliandikwa kinyume na kanuni ya 55 (12)
ambayo imetoa mamlaka kwa Spika na sio Katibu wa Bunge.

Kufuatia barua hiyo niliitwa na kuelezwa kwamba naweza kuwasilisha baadhi
tu ya marekebisho na mengine sipaswi kuyawasilisha. Kwa kuwa muda ulikuwa
umekwenda niliamua kuingia katika ukumbi wa Bunge na kujiandaa kutumia
kanuni ya 55 (11) ambayo inatoa fursa hata kwa mbunge ambaye hakutoa taarifa
kabla, kuwasilisha mabadiliko yake ukumbini kwa idhini ya Spika.

Yaliyotokea baada ya hapo mchana wa tarehe 4 Februari 2013 wengine
mliyashuhudia kwa kuwa nilipunjwa muda, nilikataliwa kuwasilisha baadhi ya
mabadiliko, nilikatishwakatishwa, nilizuiwa kusoma maelezo yangu ya nyongeza;
kinyume kabisa na kanuni na inavyokuwa kwa watoa hoja wengine hususan wa
Serikali.

Katika hali hiyo, nilimweleza wazi bungeni, Naibu Spika Job Ndugai kuwa
nitakata rufaa dhidi ya maamuzi yake yenye mwelekeo wa kuficha uozo na ufisadi
kwa kukiuka kanuni za Bunge.

Jioni ya tarehe 4 Februari 2013 Waziri wa Maji badala ya kuchangia kwa kujibu
hoja kama kanuni ya 53 (6) (c) aliwasilisha hoja tofauti kwa kutumia kanuni ya
57 (1) (c) ya kuiondoa hoja yangu isiendelee kujadiliwa kwa maelezo kwamba
“tayari kuna mpango maalum uliotengewa fedha nyingi na Serikali ya CCM na
kwa kuzingatia kuwa utekelezaji wa mpango huo unaendelea vizuri sana”.

Waziri alikiuka kanuni za Bunge kwa kuwasilisha hoja hiyo kwa kuwa kanuni
ya 57 (4) badiliko hilo lilikuwa linapingana na hoja kwa kuwa linaiondoa hoja
yenyewe na kanuni ya 58 (5) ambayo inaelekeza kwamba hoja ikishawasilishwa
anayeweza kuondoa hoja ni mtoa hoja mwenyewe tu tena kwa idhini ya Bunge.

Aidha, Waziri wa Maji alitoa maelezo yenye kulidanganya bunge, kujenga
matumaini hewa fedha za kutosha zimetengwa na utekelezaji unakwenda vizuri
sana. Hiyo ilikuwa kinyume kabisa na maelezo yake mwenyewe bungeni tarehe 10
Julai 2012, 7 Novemba 2012 na nyaraka nilizonazo za ndani ya Serikali za Januari
2013.

Pia, Waziri wa Maji hakutoa maelezo kuhusu mradi wa ukarabati na upanuzi
wa miundombinu ya Majisafi na Majitaka Jijini Dar es salaam na maeneo ya
Bagamoyo na Kibaha (Dar es salaam Water Supply and Sanitation Project-
DWSSP) uliotumia dola milioni 164.6 hata hivyo mpaka sasa katika maeneo
mengi mtandao wake maarufu kama mabomba ya Wachina, hautoi maji huku
kukiwa na upungufu katika uzalishaji, upotevu wakati wa usafirishaji, udhaifu
katika usambazaji na tuhuma za ufisadi katika matumizi.

Hakujibu pia iwapo Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) atafanya
ukaguzi maalum wa matumizi ya fedha matumizi ya bilioni 96.4 za mradi wa maji
safi na mazingira vijijini katika Jiji la Dar es salaam na Halmashauri zingine na
kuwezesha hatua za ziada kuchukuliwa kutokana na matumizi mabaya ya fedha
pamoja na kasoro zingine katika utekelezi wa Programu ya Maji Safi na Mazingira
Vijijini (RWSSP) ikiwemo katika Manispaa za Jiji la Dar es Salaam ilipaswa
kutekelezwa kuanzia mwaka 2005/2006 na kukamilika mwaka 2010/2011.

Kwa ujumla, hakueleza hatua zozote ambazo Serikali inatarajia kuchukua
kutokana na hatua tisa za haraka nilizopendekeza kwenye hoja yangu na masuala
niliyotaka yazingatiwe kutoka katika maelezo yangu ili kuboresha upatikanaji wa
maji safi na ushughulikiaji wa maji taka katika Jiji la Dar es salaam.

Tumefikaje katika hali hii?
Katika waraka wangu wa kwanza kwa mwaka 2012 kwenu (Ukweli ni Uhuru)
wa tarehe 22 Juni 2012 nilirejea mchango wangu bungeni wa tarehe 19 Juni
2012 ambapo nilihoji kwa niaba yenu namna bajeti ya nchi ya mwaka 2012/2013

ilivyokuwa haikuzingatia vipaumbele vyenye kudhibiti mfumuko wa bei nchini
na kiwango cha fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara za mzunguko na maji katika
Jiji la Dar es Salaam kuwa kidogo ukilinganisha na mipango na ahadi za Serikali.
Nilieleza hali hiyo imetokana na “udhaifu wa Rais, uzembe wa Bunge na upuuzi
wa CCM” , kauli ambayo ilinifanya nitolewe nje ya Bunge.

Niliwaeleza madaraka makubwa juu ya wabunge aliyonayo Rais kutokana na
ubovu wa katiba ya nchi ibara ya 90 na 99 kuhusu bajeti ya maendeleo na sheria
ya fedha; na hivyo madaraka ya Bunge na wabunge juu ya kufanya mabadiliko
kwenye bajeti ya nchi kukatazwa kupitia Kanuni ya 97 ya Kanuni za kudumu za
Bunge.

Nilieleza kuwa hali hiyo ilikuwa ni matokeo pia wa uzembe wa Bunge
kutokutumia ipasavyo kanuni ya 94 ya Kanuni za Kudumu za Bunge kujadili
mapendekezo ya mpango wa Serikali katika mkutano wa Bunge uliofanyika mwezi
Februari 2012.

Hivyo, nilishauri hatua ambazo Rais kwa nafasi yake ya mwenyekiti wa Baraza la
Mawaziri na Mwenyekiti wa Tume ya Mipango na kwa mamlaka yake makubwa
ya kikatiba ikiwemo ya kuwa mkuu wa nchi na kiongozi wa Serikali anaweza
kuzichukua kurekebisha udhaifu uliojitokeza katika Mpango wa Maendeleo na
Bajeti ya mwaka 2012/2013.

Niliwaahidi kuendelea kutimiza wajibu wa kibunge wa kuwawakilisha wananchi
na kusimamia uwajibikaji wa Serikali ili kuwezesha maendeleo, na katika kufanya
hivyo mwezi Oktoba mwaka 2012 niliwasilisha TENA taarifa ya hoja binafsi
kuhusu hatua za haraka za kuboresha upatikanaji wa maji safi na ushughulikiaji wa
maji taka katika Jiji la Dar es Salaam. (Taarifa hiyo nimewahi kuitoa kwa nyakati
mbalimbali toka mwaka 2011 lakini sikuwahi kupewa nafasi).

Hatimaye hoja hiyo iliingizwa katika ratiba ya Mkutano wa Tisa wa Bunge hata
hivyo tarehe 7 Novemba 2012 ikiwa ni siku moja kabla ya kuwasilisha hoja yangu
bungeni tarehe 8 Novemba 2012, Waziri wa Maji akapewa nafasi ya kuwasilisha
Kauli ya Serikali kuhusu Mpango Maalum wa kutatua tatizo la maji katika Jiji la
Dar es salaam.

Hayo yalifanyika wakati hoja yangu ilipaswa kuwa siri ya Ofisi ya Katibu wa
Bunge na uongozi wa Bunge uliruhusu kauli ya Serikali ambayo vyanzo vyangu
mbalimbali ndani ya Bunge, Serikali na CCM vilinieleza kwamba ililenga kuondoa
haja ya hoja yangu (pre-emption).

Niliomba muongozo tarehe 7 Novemba 2012 kwa kuwa pamoja na kauli hiyo
bado masuala ya msingi niliyotaka Bunge iyajadili na kufanya maamuzi yalikuwa
hayajapatiwa majibu katika kauli ya Serikali; hata hivyo sikuweza kupewa nafasi
ya kuwasilisha hoja binafsi tarehe 8 Novemba 2012, hatua iliyonifanya niwasilishe
TENA hoja hiyo tarehe 4 Februari 2013.

Kwa kuwa imeondolewa bungeni kinyemela naiwasilisha kwenu muijadili na
kufanya maamuzi mtakayoona yanafaa kwa maslahi ya umma.

Maji; kwa nguvu ya umma!.
Wenu katika uwakilishi wa wananchi,
John Mnyika (Mb)
Bungeni-Dodoma
06/02/2013
Previous Post Next Post