MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA), imekusanya asilimia 23 ya Sh8.7 trilioni zilizopangwa kukusanywa katika mwaka mzima wa fedha 2012/13 ikiwa ni makusanyo ya miezi mitatu.
Mkurugenzi Mkuu TRA, Harry Kitilya alisema jana Dar es Salaam kuwa mamlaka hiyo inaweza kuvuka malengo ya makusanyo waliyojiwekea.“Malengo yetu yalikuwa kukusanya Sh 8.7 trilioni kwa mwaka 2012/13, lakini kwa miezi mitatu tu tumeshakusanya asilimia 23 ya kiasi hicho,” alisema Kitilya.
Kitilya alisema wameshakusanya asilimia 23 ya mapato hayo kutokana na ukusanyaji huu wanaweza kuvuka lengo la asilimia 25 walilojiwekea.
“Ukusanyaji wa mapato kwa miaka sita iliyopita tulikuwa tunakusanya mapato asilimia 8.5 lakini ilipofika mwaka fedha 2011/2012 mapato yaliongezeka kwa asilimia 17, ambapo katika kipindi cha miezi mitatu wa mwaka wa fedha mwaka huu tumekusanya asilimia 23, ” alisema Kitilya .
Alisema TRA watafanya maadhimisho ya sita ya mlipakodi yatakayofanyika Novemba 7 mwaka huu, ambapo mgeni rasmi atakuwa Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Gharib Billal.
Alisema maadhimisho hayo yataambatana na utoaji tuzo kwa walipakodi waliofanya vizuri katika ulipaji kodi kwa hiari, waliochangia kiasi kikubwa cha kodi pamoja na taasisi ambazo zimeisaidia TRA katika ukusanyaji wa kodi.
Alisema tofauti na miaka mingine mwaka huu watatoa tuzo ya mwanamke ambaye ametoa mchango katika kuendesha taasisi muhimu, ambayo imesaidia akina mama kuendesha biashara na kulipa kodi.
“Jumla ya walipakodi 562 watapewa tuzo mbalimbali kama vyeti na vikombe inayo jumuisha kampuni, taasisi na walipakodi binafsi nchini, pamoja na taasisi ambazo zimesaidia TRA kukusanya kodi” alisema Kitilya.
Kitilya alisema mamlaka hiyo imelenga kutoa Sh23 milioni kwa ajili ya watoto yatima na kuisaidia Hospitali ya Wilaya ya Kisarawe kununua vitanda katika wodi ya wazazi.
“Tumelenga kuisaidia jamii kama kituo cha watoto yatima kilichopo Mbagala,Kimara na tutaisaidia Hospitali ya Wilaya ya Kisarawe kununua vitanda katika wodi ya wazazi,”alisema Kitilya.
Chanzo Mwanchi
Tags:
Business
