Rais Jakaya Kikwete akitoa salamu zake wakati wa kusimikwa askofu wa singida KKKT
Askofu mkuu kanisa la KKKT Tanzania, Dk. Alex Malasusa(mwenye fimbo) akimtambulisha kwa waumini wa kanisa hilo, askofu mteule, Dk. Alex Mkumbo baadaya kuwekwa wakfu kuwa askofu kanisa hilo,dayosisi ya kati, sherehe zilizofanyika mjini Singida.
Singida
Januari 06,2013.
RAISJakaya Kikwete ameyataka madhehebu ya dini kurejesha utaratibu wa zamani wa kukutana kujadili mahusiano yao ili kuepuka uhasama wa kidini, unaoHATARISHA amani nchini.
Dk. Kikwete alisema hayo kwenye ibada ya kumweka wakfu, askofu mteule wa kanisa la KKKT- Dayosisi kati-Singida, mchungaji Dkt Alex Mkumbo, iliyofanyika makao makuu ya kanisa hilo, usharika wa Imanuel, Singida mjini.
Alisema, masuala ya udini hapo siku za nyuma hayakuwepo hapa nchini kutokana na viongozi wa madhehebu ya dini kukutana na kumaliza tofauti zao mapema,lakini hivi sasa utamaduni huo umetoweka hali inayoweza kuchangia kutokea kwa machafuko ya udini hapa nchini.
“Nimeogopeshwa sana na hali ya kulegalega kwa hali ya amani, utulivu na usalama wa nchi yetu, hususani kipindi cha mwaka jana…naomba hali hiyo isitokee tena mwaka huu wa 2013,”alisema Dk. Kikwete na kuongeza kuwa.
“Maana hata nilipolazimika kutumia vyombo vya dola vyenye dhamana ya kutuliza ghasia, bado hali ilikuwa ngumu…lakini naamini kupitia Misikiti na makanisa mkiendeleakuhubiri waumini wenu, hali itakuwa shwari,”alisema.
Aidha Dk.Kikwete aliwaomba viongozi wa dini kuendelea kuwahubiri waumini wao kujiepusha na vurugu za udini, matumizi mabaya ya madawa ya kulevya, uvivu,biashara ya ukahaba na kupiga vita vitendo vya kuomba na kupokea rushwa, ili washiriki vema kujiletea maendeleo yao.
“Dini na serikali wote tunafanya kazi ile ile ya maendeleo…wananchi wanahimizwa kujiletea maendeleo na dini pia inahimiza waumini wake kupata maendeleo,kwa nawaomba tuendelee kushirikiana pamoja, serikali yangu inaahidi kushirikiana na madhehebu ya dini,”alisema.
Alisema utaratibu wa zamani wa viongozi wa dini walikuwa wanatumia kukaa na kujadili maswala mbalimbali ulikuwa unasaidia kutuliza ghadhabu, kuonya na kufundisha, hali aliyotaka ufufuliwe na kuhuishwa upya ili kuimarisha amani na utulivu nchini.
Kwa upande wake askofu mkuu wa kanisa la KKKT Alex Malasusa alimshukuru Rais Kikwete, kwa kutoa kauli hiyo inayowahakikishia waumini wamadhehebu yote uhuru wa kuabudu kilamtu na dini yake.
Dk. Malasusa alimweleza Rais kuwakanisa litakuwa bega kwa began a serikali,kuhakikisha amani na utulivu vinaendelea kudumu nchini,licha ya watu wachache kutaka kusababisha vurugu na uvunjifu wa amani.
Mapema baada ya kuwekwa wakfu, katika risala yake askofu Dk. Alex Mkumbo alimwomba Rais Kikwete kusaidia kurejesha shule ya wasichana ya sekondari Ruruma iliyopo wilaya Iramba, kutokana na eneo hilo kuwa kitovu cha kuanzishwa kwa dhehebu la Lutherani, kwenye dayosisi hiyo.
Dk. Mkumbo alimweleza Rais,kwa kuwa shule hiyo ilichukuliwana na CCM na yeye ndiye mwenyekiti wa taifa wa chama hicho, kanisa linaiomba ili liweze kuweka mambo mengi muhimu kwa ukumbusho wa KKKT Dayosisi ya kati.
Hata hivyo katika majibu yake, Rais aliwataka viongozi wa kanisa hilo kukutana na wenzano viongozi wa mkoa Singida, ili kumaliza kabisa tatizo hilo.