DKT.SHEIN AFUNGUA MKUTANO WA BARAZA LA BIASHARA


IMG  5452
Na Faki Mjaka-Maelezo Zanzibar        
 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein amesema Serikali yake ina dhamira ya dhati ya kuimarisha Sekta ya Viwanda Zanzibar na jitihada za kuitekeleza dhamira hiyo zimeshaanza, ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa huduma za umeme wa uhakika katika maeneo mengi ya Unguja na Pemba.
  
 Aidha Amesema Serikali inaendelea kuimarisha miundombinu ya Barabara, Bandari, Viwanja vya Ndege na sekta ya mawasiliano ya habari ili kuhakikisha wawekezaji wa Viwanda wanafanya shughuli zao kwa urahisi na ufanisi mkubwa.
 Rais Shein ameyasema hayo leo katika ufunguzi wa Mkutano wa saba waBaraza la Biashara la Zanzibar (ZBC), huko Ukumbi wa Salama katika hoteli ya Bwawani mjini Zanzibar uliohudhuriwa na Washiriki wa ndani na nje ya Zanzibar.
 Amesema pamoja na kuandaa mazingira mazuri kwa Wawekezaji wa Sekta ya Viwanda pia Serikali itawashirikisha vyema Wadau wa sekta binafsi ili watoe michango yao, uzoefu wao na hatimae kueleza matarajio yao katika kuimarisha Viwanda nchini. 
Rais Shein ambaye pia ni Mwenyekiti wa Mkutano huo amesisitiza umuhimu wa mchango wa sekta binafsi katika kufanikisha suala zima la maendeleo ya viwanda hapa nchini ambavyo vina umuhimu mkubwa kwa maendeleo ya Taifa.
 Amesema ana matumaini makubwa kwamba baada ya Mkutano huo watakubaliana kwa pamoja kuwa Zanzíbar  ina fursa nyingi za uwekezaji katika Viwanda vya aina mbali mbali, vikiwemo vinavyotumia mazao ya kilimo, mazao ya baharini na malighafi nyenginezo na hatimaye kuanza kufanyiwa kazi fursa hizo.
 “Tuna fursa kubwa ya mazao yetu kuyaongezea thamani ili, tupate faida zaidi.  Kwa hivyo, kwa mara nyengine nakutakeni nyote mtoe michango yenu kwa uwazi na bila ya khofu na baadae tuondoke hapa na maazimio, ambapo kila mmoja wetu ataweza kutekeleza kwa mujibu wa nafasi yake” Alisema Dkt Shein.
 Amefahamisha kuwa Mkutano huo ni hatua muhimu katika utekelezaji wa azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuishirikisha sekta binafsi katika kuimarisha uchumi wa nchi na ustawi wa wananchi kwa kuzingatia rasilimali zilizopo na mipango ya maendeleo endelevu.  
 Akigusia mkutano wa Baraza la Biashara uliopita, Dkt Shein amesema katika Mkutano huo alieleza lengo la Serikali la kuufanya utalii uwe na manufaa kwa wananchi wote katika dhana ya “utalii kwa wote” na kwamba Wananchi wa Zanzibar wamefahamu vizuri dhana hiyo.
 Amesema Serikali itaongeza jitihada ya kuwafahamisha zaidi wananchi ili wafahamu vizuri umuhimu wa utalii ikiwemo utalii wa ndani kwa maendeleo ya nchi kiuchumi na kijamii.
 Mkutano huo wa saba wa Baraza la Biashara Zanzibar wenye maudhui ya “Ubia na Uwekezaji kwa Maendeleo ya Viwanda, Zanzibar” unalenga kujenga mazingira mazuri yatakayopelekea kuvifufua na kuvikuza viwanda hasa viwanda vidogo vidogo, ili viweze kutoa mchango katika soko la ajira na kuinua mchango wake katika Pato la Taifa.

Previous Post Next Post