WITO umetolewa kwa taasisi za fedha nchini kutoa mikopo ya nyumba ili kuongeza ushindani na kupunguza kiwango cha riba kinachotozwa.
Hayo yalisemwa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mikopo ya Nyumba (TMRC), Oscar Mgaya alipozungumza na Mwananchi ofisini kwake jana juu ya mpango wa kupunguza kiwango cha riba kinachotozwa kwa sasa.
Wadau wengi wa mikopo ya nyumba wamekuwa wakilalamikia riba inayotozwa katika mikopo hiyo na hivi karibuni Rais Jakaya Kikwete aliziomba taasisi za fedha kupunguza kiwango hicho alipokuwa akizindua mradi wa nyumba za Shirika la Nyumba zilizopo eneo la Kibada, jijini Dar es Salaam.
“Natoa wito kwa benki nyingi zaidi kutoa mikopo ya nyumba tofauti na sasa ambapo chache ndizo zinazotoa huduma hii ili kuongeza ushindani sokoni na hivyo kupunguza kiwango cha riba ambacho hubainishwa na mwenendo wa soko,” alisema Mgaya.
Naye Ofisa Habari wa Benki ya Afrika (BOA), Patricia Nguma aliwataka waendelezaji wa miji na makazi kujenga nyumba nafuu ili kuwanufaisha wateja wengi zaidi na mikopo hiyo kwani wao hutoa kulingana na mahitaji ya mteja na si vingineyo.
Huduma ya mikopo ya nyumba ni ngeni kwa Watanzania wengi hivyo elimu zaidi inahitajika ili kujenga ufahamu kwa wananchi na Benki Kuu inajipanga kufanikisha zoezi hilo.
“Ni lazima tupige hatua katika soko na huu ni mwanzo wa soko la mikopo ya nyumba, hapo baadaye tutajipanga ili tuwafikie wateja wengi zaidi,” alifafanua Mgaya.
Alisema mfumuko wa bei na udanganyifu wa taarifa za baadhi ya wateja ni miongoni mwa changamoto nyingi zinazoikabili huduma hii hapa nchini hivyo kupelekea riba kufikia asilimia 18.
Aidha, alisema Serikali ina jukumu la kushughulikia suala la kiwango kikubwa cha riba kwani kwa namna moja au nyingine imekuwa ikichangia kubainisha hasa pale inapotoa hawala na amana za Serikali ambazo ndiyo msingi wa riba ya soko.
Tags:
Business
